2013-01-03 10:13:59

Barua ya wazi kwa Wazazi wa Mapadre na Waseminari


Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari amewaandikia barua ya wazi mama wazazi wa Mapadre na Majandokasisi, akiwaomba kutafakari kwa kina dhamana ya Bikira Maria aliyepewa upendeleo wa pekee hata akakubali kumzaa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na Kuhani mkuu.

Bikira Maria kwa njia ya utii na unyenyekevu wake, aliweza kushiriki katika Mpango wa Kazi ya Ukombozi, kiasi kwamba, akawa ni Mama wa Mungu, Mlango wa mbingu na sababu ya furaha ya waamini. Kwa upande wake, Kanisa linawaangalia kwa upendo na shukrani kubwa, akina Mama wote wa Mapadre na Waseminari, wanaoendelea kushiriki kikamilifu katika majiundo ya watoto wao: kiroho na kimwili, ili waweze kjujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; wakitambua kwamba, watoto wao kwa njia ya Sakramenti ya araja takatifu wamekuwa ni marafiki wa Kristo, wanaomwezesha kuendelea kuwepo kati ya wafuasi wake kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa.

Kardinali Piacenza anasema kwamba, hili ni Fumbo kubwa kwa Padre kuwa ni Kristo mwingine, licha ya mapungufu na kasoro za kibinadamu zinazoendelea kumwandama katika maisha na utume wake. Anakuwa ni daraja linalowaunganisha waamini pamoja na Kristo aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka siku ya tatu kama yanenavyo Maandiko Matakatifu. Mapadre ni viongozi wa waamini katika Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na wanapofundisha Imani na Kweli za Kikristo. Matendo yote haya ni mwendelezo wa kazi ya Ukombozi iliyoanzishwa na Yesu Kristo mwenyewe.

Kardinali Piacenza anabainisha kwamba, Familia ni kitovu cha Sala na upendo; ni shule ya kwanza ya Imani na kitalu cha miito mitakatifu ndani ya Kanisa; hasa pale Familia za Kikristo zinapokuwa imara katika tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kiroho. Huu unakuwa ni udongo mzuri unaoweza kukoleza utakatifu wa maisha miongoni mwa Mapadre na waamini katika ujumla wao. Wazazi, walezi na ndugu na Jamaa washiriki kikamilifu katika majiundo ya watoto wao ambao ni Mapadre au bado wako katika majiundo ya kikasisi.

Wawahimize watoto wao kutekeleza wajibu na dhamana yao ya Kipadre, wakiwaachia uhuru wa kuweza kulijenga Kanisa na kamwe wasiwe ni vikwazo vya watoto wao Mapadre. Wawasindikize kwa sala na sadaka yao ya kimama; ili waweze kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa ukamilifu zaidi na kwa ajili ya mafao ya Familia ya Mungu. Wawasaidie watoto wao katika mapambano ya Kiimani, wakijiunganisha na Sadaka ya Yesu Kristo pale Msalabani.

Kardinali Mauro Piacenza anawakumbusha akina Mama wa Mapadre na Waseminari kwamba, ulimwengu wa leo ni tambara bovu linalojionesha kwa namna ya pekee katika kumong'onyoka kwa maadili na utu wema; watu kuendelea kuelemewa na mawazo mepesi mepesi pamoja na tabia ya ukanimungu. Ni changamoto ambazo pia ziko mbele ya Mapadre na Waseminari katika majiundo yao ya Kikasisi.

Mama wa Mapadre wasikate tamaa kuwasindikiza watoto wao katika sala na majitoleo; wawaombee ili waweze kudumu katika uaminifu, daima wakichuchumilia utakatifu wa maisha. Kanisa linawaombea Mama wote wa Mapadre ambao wamekwisha kutangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele kwa kazi njema waliyoifanya kwa ajili ya Kanisa. Bikira Maria Mama wa Mungu awe Mwombezi wao wa daima katika hija ya maisha yao kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.