Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI: muasisi wa mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amepitisha hati ya Mtumishi wa Mungu Papa
Paulo wa Sita kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa kutambua fadhila za kishujaa zilizooneshwa
na Mtumishi huyu wa Mungu katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa.
Giovanni Battista
Montini, alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897, huko Concesio, Brescia, Italia. Alipadrishwa
tarehe 29 Mei 1920. Baada ya kufanya utume Jimboni Brescia, alihamishiwa Jimboni Roma
kati ya Mwaka 1920 hadi mwaka 1922, akajiendeleza katika masomo ya Sheria za Kanisa
na Sheria za Kijamii kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.
Mwaka 1923
akaanza utume wake wa Kidiplomasia katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Akatumwa kutekeleza
utume huu nchini Poland na baadaye, mwaka 1924 akarudishwa Italia kuendelea na utume
wa kusaidia Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Italia, utume ambao aliendelea
kuutekeleza hadi mwaka 1933.
Tarehe 13 Desemba 1937 akateuliwa kuwa Katibu
mkuu msaidizi wa Vatican na baadaye tarehe 29 Novemba 1952 akateuliwa kuwa Katibu
mkuu wa mambo maalum mjini Vatican. Tarehe Mosi, Novemba 1954, Baba Mtakatifu Pio
wa kumi na mbili akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano. Tarehe 15 Desemba
1958 Giovanni Battista Montini akateuliwa kuwa Kardinali na Baba Mtakatifu Yohane
wa Ishirini na tatu.
Tarehe 21 Juni 1963 akachaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu
Petro. Tarehe 29 Septemba 1963 akafungua sehemu ya pili ya Maadhimisho ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, uliohitimishwa hapo tarehe 8 Desemba 1965, kwa Maadhimisho
ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Tarehe Mosi, Januari 1968 kwa
mara ya kwanza akaadhimisha Siku ya Kuombea Amani Duniani. Tarehe 24 Desemba 1974
akafungua lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kama ishara ya kuzindua Mwaka wa
Imani. Akafariki dunia hapo tarehe 6 Agosti 1978, akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel
Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.
Papa Paulo wa sita ni kiongozi wa Kanisa
aliyethubutu kufanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia
ya nyaraka, hija za kichungaji ndani na nje ya Italia pamoja na fursa ya kukutana
na viongozi mbali mbali wa kidini na kiserikali, kama kielelezo cha majadiliano ya
kina kati ya Kanisa: Dini, Madhehebu, Serikali na Tamaduni.
Papa Paulo wa sita
katika Mafundisho yake ya Jumla kwa njia ya Nyaraka anakazia kwa namna ya pekee umuhimu
wa Kanisa, kukuza na kudumisha majadiliano ndani ya Kanisa lenyewe; Kanisa na Ulimwengu.
Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, ndiyo maana wakati wa maadhimisho ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali
kwa ajili ya kuombea mafanikio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambayo mwaka huu
Mama Kanisa anasherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu ulipozinduliwa.
Alifanya
mabadiliko makubwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho; akakazia masuala
ya kijamii pamoja ya kuyataka Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kufanya mabadiliko
ya ndani mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyejikita
katika azma ya Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu Paulo wa sita, alikuwa ni Kiongozi
wa kwanza kabisa wa Kanisa Katoliki kufanya hija za kichungaji nje ya Italia. Kwa
mara ya kwanza alisafiri hadi Nchi Takatifu, kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 6 Januari
1964, safari ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuanzisha majadiliano
ya kidini na Wayahudi. Alikuwa ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa kuhutubia Baraza kuu
la Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
Alijitahidi kufanya hija za kichungaji
nchini Uturuki, Colombia, Uswiss, Mashariki ya Mbali, bila kusahau hija yake ya kichungaji
Kampala, Uganda kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969, hapa kwa namna
ya pekee, alilitaka Kanisa Barani Afrika kujikita kwanza katika utume wa kimissionari
kwa kutambua kwamba, ulikuwa umefika wakati kwa Waafrika wenyewe kuwa ni Wamissionari
ndani ya Bara la Afrika, mwanzo wa mchakato wa kuanzishwa kwa Mashirika ya Kitawa
na Kimissionari Barani Afrika; matunda yake yanaonekana.
Baba Mtakatifu Paulo
wa sita ni kiongozi aliyetekeleza utume na dhamana yake hata kwa njia ya kukutana
na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Kisiasa, kama kielelezo cha Kanisa kutaka
kuendeleza majadiliano ya kina na Serikali kwa ajili ya mafao ya wengi. Hiki kilikuwa
ni kipindi chenye utata mkubwa kutokana na kuwepo kwa Vita Baridi. Alifanya pia mkutano
na viongozi wa kidini kama mwendelezo wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni.
Baba
Mtakatifu Paulo wa sita, alileta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa
kwa kuanzisha tume mbali mbali zilizokuwa na wajibu wa kuendeleza mawasiliano, majadiliano
ya kidini na kiekumene; Sinodi za Maaskofu kama jukwaa pana zaidi la kusali, kujadili
na kupendekeza vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa baada ya kusoma alama za nyakati.
Alitoa nafasi kubwa kwa waamini walei kutekeleza wajibu wao kwa kuanzisha tume ya
walei; tume ya uchumi, fedha na mipango ya Vatican, Idara ya takwimu za Kanisa.
Papa
Paulo wa sita, ni muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani, inayofanyika
kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari. Alianzisha pia Tume ya Kitaalimungu Kimataifa;
Kanuni na taratibu za maadhimisho ya Liturujia ya Kipapa. Kwa ujasiri mkubwa alifuta
uwepo wa Jeshi lenye silaha mjini Vatican na kuamua kwamba, Vatican italindwa na Wanajeshi
kutoka Uswiss wanaojulikana kama Swissguards.
Kwa kuguswa na umaskini wa watu
pamoja na kupania kulishirikisha Kanisa katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo
endelevu, alianzisha Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor
Unum, ambacho hadi leo hii ni chombo makini cha huruma, upendo na ukarimu wa Kanisa
Katoliki kwa watu wanaoonesha kiu ya maendeleo na wale wanaokumbwa na maafa asilia
sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anamkumbuka
kwa namna ya pekee kama Papa aliyejikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini,
kiekumene, kitamaduni na kiserikali, akionesha umuhimu wa Kanisa kuwa ni chachu ya
majadiliano haya ili kutoa fursa kwa watu mbali mbali kuweza kukutana na Kristo kwa
njia ya Kanisa. Aliwahimiza: ufahamu, mabadiliko na majadiliano, ili kufahamu asili
ya Kanisa, utume na dhamana yake pamoja na hatima ya Kanisa kwa siku za usoni. Kanisa
halina budi kuwa wazi kwa ulimwengu ili kuleta mabadiliko ya ndani yanayokusudiwa
kwa kujikita katika utakatifu wa maisha.
Ni kiongozi aliyetamani kwamba, maisha
yake yawe ni ushuhuda wa ukweli, unaofanyiwa utafiti wa kina, kuhifadhiwa pamoja na
kuungwama katika ukweli. Alikuwa ni mwalimu mahiri wa kweli za Kiinjili, aliyekazia
majiundo makini kwa watoto wa Kanisa; akawahimiza viongozi wa Kanisa kuwekeza katika
majiundo makini ya vijana, ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kina na ulimwengu
ambao una magumu na changamoto zake.
Kwa ufupi, huyu ndiye Mtumishi wa Mungu
Baba Mtakatifu Paulo wa sita, anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri na Mama Kanisa
wakati wowote kuanzia sasa.