2013-01-02 15:20:33

Mtoto wa mkulima Mizengo Pinda atangazwa kuwa ni Mfalme wa Nyuki Tanzania!


Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amepewa Tuzo ya Heshima ya Mwaka 2012 ya Mkoa wa Katavi katika vipengele viwili vya Utawala Bora na Uhamasishaji wa ufugaji nyuki. Waziri Mkuu alipokea tuzo hizo Jumanne, Januari Mosi, 2013 kwenye hafla ya kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji mjini Mpanda, mkoani Katavi.

Akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya kutangaza majina ya watunukiwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alisema mkoa wa Katavi umeamua kuanzisha mfumo wa utoaji wa Tuzo ya Mkoa kwa lengo la kuwatambua, kuwatia moyo na kuwapa motisha wananchi na watumishi wa umma waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tuzo hii itaendelea kutolewa kila mwisho wa mwaka... Tumeamua kufanya hivi ili kuamsha ari kwa wengine kufanya vizuri zaidi mwaka unaofuata,” alisema. Sekta zilizopewa tuzo ni mapato na kodi za Serikali, utawala bora, uchumi na maendeleo, Ulinzi na usalama, mipango miji, mawasiliano na teknolojia, ufugaji nyuki na hifadhi ya mazingira, elimu, kilimo na mifugo, michezo, usafirishaji na huduma za jamii.

“Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatunukiwa tuzo ya utawala bora, siasa safi na ushiriki katika shughuli za maendeleo ya wananchi wa jimbo lake la Katavi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika kikamilifu,” alisema. “Tuzo ya pili ni ya kumtambua kuwa mfugaji nyuki na mhamasishaji kichocheo wa kitaifa wa ufugaji nyuki. Sisi wana-Katavi tunakutambua kama Mfalme wa Nyuki nchini,” aliongeza.

Wengine waliopewa tuzo katika hafla hiyo ni Bw. Deus Assenga, Bw. Michael M. Tarimo wa M.M (2001) Group Ltd na Bw. Shabir Hassanali Walimohamed ambao walitambuliwa kama Walipakodi Bora Mkoa wa Katavi mwaka 2012 kwenye kipengele cha Mapato na Kodi za Serikali.

Wengine ni Bw. Paschal Kweya aliyepewa tuzo katika ubunifu wa usafi na hifadhi ya mazingira Mkoa wa Katavi ambaye aliiwezesha Halmashauri ya Mji kuwa mshindi mara mbili mfululizo 2011 na 2012.

Waliotunukiwa tuzo kwenye kipengele cha mawasiliano na teknohama ni Bw. Majaliwa Rubuye ambaye alibuni tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda yenye anwani ya na kuweza kuweka daftari la mkulima katika mtandao huo. Bw. Ignas Kikwala ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii alibuni machapisho na kuandaa gazeti la Mpanda Leo ambalo hutolewa kila baada ya miezi mitatu. Hadi sasa ametoa matoleo sita.

Walioshangiliwa zaidi kwenye utaoaji tuzo hizo ni vijana watatu ambao walishiriki mashindano ya Maisha Plus wakitokea mkoa wa Katavi na wakafanikiwa kufika fainali za mashindano hayo. Vijana hao ni Bi. Theresia Zacharia ambaye amepata nafasi ya kujiunga na JKT moja kwa moja bila kufanyiwa usaili; Bw. Lucas Martin na Bw. Gabriel Luvinga.

Waliotunukiwa tuzo kwenye sekta ya elimu ni wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa darasa la saba ambao wanatoka kwenye shule za kawaida za Vijijini katika wilaya ya Mpanda na wamechaguliwa shule za wenye vipaji maalum. Vijana hao ni Benjamin Busagala (kutoka S/M Majimoto) ambaye amechaguliwa kwenda Sekondari ya Mzumbe na Christina Boniface kutoka S/M Ikuba ambaye amechaguliwa kwenda sekondari ya wasichana Tabora








All the contents on this site are copyrighted ©.