Jipangeni vyema kukabiliana na changamoto za Mwaka 2013
Imeelezwa kuwa dunia sio mbaya bali wabaya ni wanadamu ambao tupo hapa duniani hivyo
cha kufanya ni kumrudia mwenyezi mungu ili abadilishe mienendo yetu. Kauli hiyo imetolewa
na Padre Chesco Peter Msaga, Makamu Askofu Jimbo Katoliki Dodoma wakati wa ibada ya
mkesha wa mwaka mpya 2013, ibada iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa
Damu Azizi, Kisasa Medelii, Dodoma.
Padre Msaga amesema wanadamu tumekuwa
na kasumba ya kulalamika kuwa dunia ni mbaya badala ya kuangalia ni kwanini inakuwa
mbaya hali ambayo imekuwa ikitafsiriwa tofauti na inavyoonekana. Kuna haja ya watu
kujikita katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
wa dhati; changamoto ya kuwa kweli ni wajenzi wa amani inayopata chimbuko lake katika
moyo wa mtu; watu washinde ubaya kwa wema!
Alisema sisi ndio tunaopita hapa
duniani na sio watu wengine hivyo kama dunia ni mbaya tutambue kuwa wanaoifanya kuwa
mbaya ni sisi wenyewe hivyo hatuna budi kutafuta dawa ya kuweza kuifanya ikawa sio
mbaya.
“ Sisi ndio tunapita hapa duniani na sio wengine kinachotakiwa kufanyika
ni sisi kubadilika kutoka ubaya kwenda uzuri na sio vinginevyo” alikazia Padre Msaga.
Hata
hivyo aliwataka waamini na Taifa kwa ujumla kuangalia ni kitu gani ambacho wamekirimiwa
na Mwenyezi Mungu kwa kipindi chote cha mwaka 2012 na kuweza kumrudishia Mungu sifa,
utukufu, heshima na shukrani kwa yote aliyowatendea na kuwakirimia.
Alisema
kwa kipindi cha mwaka 2012 wapo wengi ambao wamekumbwa na magonjwa, ajali, wengine
wapo magerezani wengine wamekufa lakini yote hayo ni mapenzi yake Muumba hivyo sisi
ambao tumefanikiwa kuuona mwaka huu mpya wa 2013 tumshukuru Mwenyezi Mungu kwani yeye
ndiye mwingi wa rehema na neema zake ametukirimia sisi.
“Hebu tujiulize ni
mara ngapi tunatumekaa na kumwambia Mwenyezi Mungu asante kwa yote uliyotujalia kwa
mwaka mzima” aliuliza Padre Msaga. Sasa watu wamekuwa na kauli ya kuwa siku zinakwenda
mbio hapana sio hivyo! Bali ni sisi wenyewe tunaokwenda mbio katika maisha na mahangaiko
yetu ya kila siku na kumsahau Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo cha yote tuyapatayo
na tuliyonayo.
Aidha katika ibada hiyo pia aliwaomba waamini walioshiriki kuwaombea
wale wote ambao wako safarini, wagonjwa, waliopo magerezani, walinzi, madaktari, walimu,
na wote wale wanaofanya kazi kwa ajili ya wengine ili Mungu awape moyo mkuu na wa
kujituma zaidi katika shughuli zao na katu wasikate tamaa ili kujenga Taifa la Tanzania
ambalo linasifika kwa kuwa kisiwa cha amani, ingawa kuna dalili kwamba, amani hii
ikatoweka ikiwa kama wananchi hawatasimama kidete kupinga chokochoko zote zinazotishia
misingi ya haki, amani na utulivu; daima wakijikita kutafuta mafao ya wengi.
Padre
Msaga pia hakuwa nyuma katika kuwakumbusha waamini kuhakikisha kuwa wananunua ving`amuzi
ili waweze kupata matangazo angavu na yenye muonekano mzuri kwa kutumia njia ya digitali
na kuondokana na mfumo wa analojia.