2013-01-01 09:36:23

Watanzania jengeni utamaduni wa amani, upendo na mshikamano, vita haina macho!


Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Mama Kanisa anatambua na kuthamini amani katika maisha, ustawi na maendeleo ya watu kwani amani ni jina jingine la maendeleo kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Paulo wa Sita. RealAudioMP3

Lakini kwa bahati mbaya au kwa makusudi mazima, kuna watu ndani ya Jamii wanachezea amani ambayo ikishatoweka inakuwa ni vigumu sana kupatikana kama uzoefu na mang’amuzi yanavyoonesha kwa nchi nyingi.

Kwa siku za hivi karibuni anasema Askofu mkuu Lebulu, Tanzania imeshuhudia mfumuko wa kasi ya ajabu ya vitendo vinavyoashilia kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na utulivu. Malumbano na kashfa za kidini; athari za misimamo mikali ya kiimani; utovu wa nidhamu, maadili na baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao ni mambo ambayo yanahatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Vitendo hivi vimeanza kupelekea baadhi ya waamini kujenga hisia za kujihami na kutaka kulipiza kisasi pale tu matukio kama haya yatakapojitokeza kwa mara nyingine, hisia za namna hii ni hatari zinaweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa.

Askofu mkuu Lebulu anabainisha anasema Yesu Kristo ni mfalme na chemchemi ya amani nawataka wafuasi wake wasilipize ovu kwa ovu bali waushinde ubaya kwa kutenda mema, lakini pia watambua dhamana ya kusimama kidete: kutetea, kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu na upatanisho wa kweli kwani wanachangamotishwa kuwa ni wajenzi wa amani.

Wakati huu vitendo vya uvunjifu wa amani vinapoendelea kuongezeka siku hadi siku, kuna haja kwa watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kujiuliza maswali ya msingi: ni mambi yepi yanayopelekea kinzani, mgogoro na misimamo mikali ya kiimani?

Kuna haja ya watu kujenga utamaduni wa majadiliano, unaosimikwa katika heshima na kuthaminiana; utii wa sheria, nidhamu na maadili mema, kwani vita haina macho! Watu wasitumie imani kujenga jazba kwa ajili ya mafao yao binafsi, badala yake, watu watambue umuhimu wa kujadiliana, kusameheana na kupatana pale kunapotokea chokochoko na hali ya kutoelewana katika Jamii jambo ambalo ni la kawaida kabisa.

Askofu mkuu Lebulu anaonya kwamba, Wakristo hawataendelea kukaa kimya na kuona Makanisa yao yakitiwa kiberiti! Lazima watahoji na hapa sheria na vyombo vya dola vinapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Jamii nzima katika kulinda raia na mali zao. Ukweli na uwazi vitawale na kamwe baadhi ya watu wasiruhusiwe kushika sheria mikononi mwao.

Watanzania wajifunze kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa; watu waachane na tabia ya kutaka kulipizana kisasi, watambue kwamba, wote ni ndugu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; utu na heshima ya kila mtu ithaminiwe na kuheshimiwa ili kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.