Kanisa Katoliki katika mchakato wa kulinda na kutetea haki msingi za binadamu!
Baraza la Kipapa la Haki na Amani tangu kuanzishwa kwake mara tu baada ya maadhimisho
ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, limekuwa mstari wa mbele katika kulinda, kusimamia
na kutetea haki msingi za binadamu, kama ambavyo zimebainishwa katika Azimio la Haki
Msingi za Binadamu, lililotolewa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.
Baba Mtakatifu
Yohane wa Ishirini na tatu ni kati ya viongozi wa Kanisa Katoliki walioweka bayana
umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu zinazojikita
katika utu wa binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu mintarafu sheria za kimataifa na
kitaifa. Hizi ni kanuni msingi zinazobainishwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa,
yanayopania kuyatakatifuza malimwengu.
Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu ni kati ya
mambo ambayo kwa sasa yako hatarini kutokana na sababu mbali mbali, ndiyo maana kuna
haja kwa wadau mbali mbali kusimama kidete kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu,
utu na heshima yake vinalindwa na kudumishwa sehemu mbali mbali za dunia.
Tamko
la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni matokeo ya tafakari ya kina iliyofanywa
na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu athari zilizokuwa zimesababishwa na vita
kuu ya kwanza na ile ya pili ya dunia; ambapo kuna watu wengi walipoteza maisha na
mali; utu na heshima yao vikawekwa rehani. Walitaka kuweka kanuni msingi ambazo zimengefuatwa
na Jumuiya ya Kimataifa.
Hizi ni haki ambazo zinafumbatwa katika uhuru, haki
na amani duniani. Huu ni urithi wa binadamu wa nyakati zote na mahali pote bila ubaguzi,
kwani zinapata chimbuko lake kutoka kwa binadamu mwenyewe aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu na kwamba ni sehemu ya asili ya binadamu.
Ni mchango wa Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani alioutoa hivi karibuni kwenye
Kongamano la Kimataifa lililokuwa linajadili kuhusu dhamana ya Kanisa Katoliki katika
kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwa kutambua kuwa haki hizi zinafumbata
utu wa mtu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida
yanapomsibu kadiri ya mpango wa Mungu.
Tangu mwaka 1948 haki hizi zilipotangazwa
na Umoja wa Mataifa, Kanisa limeendelea kuzipigania ili ziweze kutekelezwa na Jumuiya
ya Kimataifa na wala zisibaki kwenye makabati tu, kama kumbu kumbu ya nyaraka za kale.
Baba
Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu, aliguswa kwa namna ya pekee na kinzani, wasi
wasi na woga uliokuwa umetanda wakati wa Vita Baridi sanjari na ujenzi wa Ukuta wa
Berlin, Ujerumani, alipoandika Waraka wa Kichungaji, Amani Duniani, Pacem In
Terris, akakazia mambo makuu manne kama vigezo vya kudumisha haki msingi za
binadamu: amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi
mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu, hivyo
zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda
sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu.
Hii ni haki ya kuishi, kupata
huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo
wa maisha; haki za kicuhumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia
sheria na kanuni zilizopo.