Idadi ya watanzania katika kipindi cha miaka 44 imeongezeka kwa zaidi ya watu millioni
33!
Nashukuru kwa kunialika kuja kushiriki kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria la
kutangaza matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Haya ni matokeo
ya kazi ya kuhesabu watu iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi
4 Septemba, 2012.
Ndugu wananchi; Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi za dhati kwa wale wote waliofanikisha zoezi la kuhesabu watu na wale waliokamilisha
uchambuzi unaotuwezesha leo kutangaza idadi ya Watanzania ilivyo sasa. Kwanza kabisa
napenda kutambua Kamati ya Taifa ya Sensa iliyoongozwa na Mheshimiwa Mizengo Peter
Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Idi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti upande wa
Zanzibar. Nawashukuru kwa uongozi wao mzuri ambao matunda yake ndiyo haya yanayotukusanya
leo. Pia nawashukuru wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya nchini.
Pili, napenda kuwatambua viongozi na wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri
ya Muungano chini ya uongozi wa Mama Albina Chuwa na wenzao wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu
wa Zanzibar chini ya uongozi wa Ndugu Mohammed Hafidh Rajab. Nawapongeza kwa umahiri
wao katika kuongoza, kuratibu na kisimamia utekelezaji wa jukumu lenyewe la kuhesabu
watu. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote ndiyo waliokabidhiwa kazi ngumu ya kutengeneza
mipango na taratibu za kufanya zoezi lenyewe. Walitayarisha madodoso, kuyachapisha,
kuyasambaza, kuteua watu wa kuhesabu watu na wasimamizi wao. Waliwafundisha wajibu
wao na kuwasimamia katika utekelezaji wao. Ni wao pia waliohakikisha kuwa madodoso
yote yanakusanywa na uchambuzi unafanywa mpaka sasa tuko tayari kutangaza matokeo.
Nawatambua na kuwashukuru makarani wa sensa waliopita nyumba kwa nyumba kuhesabu watu
na kukusanya taarifa mbalimbali kwa mujibu wa madodoso waliyokuwa nayo. Tunatoa shukrani
na pongezi maalum kwao kwa sababu ni wao hasa waliowezesha kupatikana taarifa itakayotangazwa
leo na nyingine zitakazofuatia siku za usoni. Kama si wao tusingekusanyika hapa
leo. Nawapongeza kwa umakini wao na moyo wao wa uvumilivu na uzalendo. Haikuwa kazi
rahisi kwa ukubwa wa kazi yenyewe. Pia, walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa
ni pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na mazingira magumu ya kufanyia kazi kama vile
ya usafiri. Lakini pia kulikuwa na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wanaoulizwa.
Baadhi hawakutoa ushirikiano unaotakiwa. Yalikuwepo pia matatizo ya kupata huduma
stahiki za kufanyia kazi na hasa posho. Nafahamu kuwa wapo bado wanaodai stahili
zao. Hazina wamekiri hilo na kuahidi watalimaliza haraka.
Ndugu wananchi; Kufanya
sensa ni kazi kubwa na ghali sana. Hata hivyo nchi zote duniani hufanya sensa kwa
sababu ya umuhimu wake. Kupitia Sensa, hupatikana taarifa muhimu za kutumiwa na Serikali
kupanga mipango ya maendeleo ya nchi na jinsi ya kuhudumia wananchi. Taarifa hizo
hutumika na wadau mbalimbali katika shughuli zao za kuwahudumia wanadamu. Ndiyo maana
madodoso yalikuwa na mambo mengi na ndiyo maana tumeambiwa kuwa taarifa ya leo ni
ya mwanzo tu. Zipo taarifa zitakazofuatia zenye uchambuzi wa mambo mbalimbali. Naomba
tuwe na subira kwa taarifa mbalimbali tunazozitaka, kwani tutazipata wakati wake
utakapofika. Kwa niaba yenu niwaombe wahusika wafanye kila wawezalo kuhakikisha kuwa
taarifa hizo zinapatikana kwa wakati uliopangwa.
Ndugu Wananchi; Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawatambua watu wengine wafuatao: Wa kwanza ni Hajat Amina
Mrisho, Kamishna wa Sensa ambaye tulimkabidhi jukumu la kutoa uongozi wa kisiasa katika
kazi ya kuhesabu watu na kuwa kiungo kati ya wataalamu na uongozi wa Serikali. Vile
vile, tulimpa kazi ya kusaidia kufikisha ujumbe pande zote ili kuona kuwa mambo yanakwenda
vizuri. Bahati nzuri mwenyewe ni mjuzi wa masuala ya takwimu. Alitokea huko kabla
ya kumchukua na kumleta katika shughuli za uongozi wa kisiasa. Hivyo, kazi ilikuwa
mikononi kwa mwenyewe.
Namshukuru kwa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Anao mchango mkubwa katika mafanikio haya. Wa pili ni wananchi wa Tanzania. Nawashukuru
kwa ushirikiano wao. Kabla na wakati wa Sensa, kulikuwa na purukushani na maneno
mengi ya upotoshaji na kutishia kuvuruga zoezi lenyewe. Wapo wenzetu walioamua kuendesha
kampeni ya kutaka watu wasusie. Wapo walioamua kufanya maandamano na mikutano ya
siasa wakati huo na jitihada zote za kuwasihi wasubiri siku 14 zipite walizipuuza.
Wakati mwingine unashindwa kuelewa baadhi yetu tuna dhamira gani katika kujihusisha
na shughuli za siasa? Hivi inakuwaje washindwe kutambua umuhimu wa kuhakikisha jambo
kubwa kama hili linafanikiwa? Hivi zoezi la sensa lisipofanikiwa kiongozi wa siasa
au wa dini unanufaika nini? Ndiyo maana nawashukuru sana wananchi kwa ushirikiano
wao uliofanya njama za kuvuruga zoezi kushindwa.
Ndugu wananchi; Wa tatu
ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya kwa kufanikisha zoezi la Sensa katika
Mikoa na Wilaya zao. Nawashukuru Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kwa uongozi
wao mzuri. Wa nne ni viongozi wa kijamii wakiwemo wa vyama vya siasa, madhehebu
ya dini na wa kimila waliosimama kidete kuhamasisha wafuasi wao kushiriki katika zoezi
la Sensa ya Watu na Makazi. Tunawashukuru kwa mchango wao muhimu. Wa tano ni wamiliki
wa vyombo vya habari na wana habari. Nawashukuru kwa kufanya kazi kubwa na nzuri
ya kuhamasisha na kuelimisha jamii katika kipindi chote cha utekelezaji wa zoezi la
Sensa. Wito wangu kwenu ni kwamba, endeleeni kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya
taarifa za Sensa kwa maendeleo ya taifa letu. Wa mwisho, lakini siyo kwa umuhimu,
nawashukuru sana washirika wetu wa maendeleo wakiwemo UNFPA, DFID, JICA, CIDA na Benki
ya Dunia kwa mchango na msaada wao mkubwa. Nawashukuru Wenzetu hawa wametupa ushirikiano
mkubwa uliotuwezesha kufanikisha zoezi la Sensa hadi kufikia hatua hii ya sasa ya
kutoa matokeo ya awali. Naomba washirika wetu wa maendeleo waendelee kushirikiana
nasi kukamilisha kazi hii na pia katika kuimarisha sekta ya takwimu nchini.
Ndugu
wananchi; Baada ya kusema maneno hayo sasa nipo tayari kuzindua rasmi matokeo ya
awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Kwa heshima na unyeyekevu mkubwa
natangaza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia
Agosti 26, 2012, Tanzania ina watu 44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434
na Zanzibar kuna watu 1,303,568. Katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002 tulikuwa milioni
34.4 hivyo tumeongezeka kwa watu milioni 10.5 ongezeko ambalo ni sawa na asilimia
2.6 kwa mwaka. Naomba taarifa hizi zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa ambayo ni
kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Ndugu Zangu; Hii ni Sensa ya nne kufanyika
nchini tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964. Sensa ya kwanza
ilifanyika mwaka 1967 ambapo nchi yetu ilikuwa na watu 12,313,054. Tanzania Bara
ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo, katika miaka
45 tangu Sensa ya kwanza na hii, Watanzania wameongezeka kwa watu milioni 33.
Ndugu Wananchi; Kama kasi ya ongezeko la watu la asilimia 2.6 halitapungua
ifikapo mwaka 2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6. Inawezekana idadi hiyo
ikaonekana kuwa siyo tatizo la kuumiza kichwa kwa nchi kubwa kama yetu, lakini ni
mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na uchumi kuwahudumia. Inabidi pawepo na mikakati madhubuti
na ionekane katika mipango ya maendeleo kuanzia sasa jinsi ya kuhudumia watu hao 51.6
na zaidi ya hao miaka inayofuata. Kwa familia, lazima tutambue umuhimu wa kupanga
uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka sana. Kwa ujumla hatuna budi kufanya kazi
kwa bidii zaidi na nguvu zaidi. Asanteni sana kwa kunisikiliza.