Yesu Kristo Mfalme wa Amani awajalie watu wa mataifa kushinda kishawishi cha chuki,
uhasama, magovi na kukumbatia misingi ya haki, amani na upendo wa kidugu!
Kanisa katika kipindi hiki cha Noeli linaendelea kusali kwa ajili ya kuombea haki
na amani huko Mashariki ya Kati kutokana na hali ngumu ya maisha: kisiasa, kidini
na kijamii, changamoto kwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali, kushiriki katika
ujenzi wa misingi ya haki na amani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini
inapaswa kudumishwa na wanadamu.
Kanisa linamwomba Mtoto Yesu aliyezaliwa
kati ya maskini na wadhambi: awasaidie na kuwafariji wote wanaoteseka kiroho na kimwili
na kwamba, watu wadhamirie kuanza mchakato wa uejnzi wa tunu ya msamaha, ukweli na
upatanisho. Siku kuu ya Noeli, ni mwanzo wa Habari Njema ya Wokovu inayoletwa na Yesu
Kristo Mkombozi wa dunia.
Ni maneno yaliyotolewa na Patriaki Fouad Twal wa
Yerusalem wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli mjini Bethlehemu alikozaliwa
Yesu. Fumbo la Umwilisho, linapata utimilifu wake katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka,
yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ni Fumbo ambalo ni kielelezo makini cha utimilifu
wa kazi ay uumbaji na ukombozi inayoletwa na Yesu Kristo.
Mtoto Yesu amezaliwa
kwa ajili ya maskini na wadhambi; wanaoteswa na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana
na imani na hali yao ya maisha: Yesu ni kwa ajili ya wote ambao bado hawajapoteza
matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu. Anamkirimia na kumrudishia mwanadamu utu na heshima
ya kuitwa tena mwana mpendwa wa Mungu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii
ndiyo ile sura iliyokuwa imechakaa kutokana na uwepo wa dhambi. Yesu Mwana wa Mungu
anakuja ulimwenguni kutangaza sheria mpya inayosimikwa katika upendo kwa Mungu na
jirani.
Ni kielelezo makini cha matumaini yasiyodanganya kamwe na mwaliko
wa kuendeleza ule mchakato unaowaunganisha wote ili waweze kujisikia kuwa ni ndugu
wamoja kwani wameumbwa na Mwenyezi Mungu, tofauti zao za kidini, kitamaduni, kisiasa
na kiuchumi ni utajiri kwa ajili ya kusaidiana kwa hali na mali na wala hazipaswi
kuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kisiasa, kijamii na kidini.
Yesu
amekuja ulimwengu ili kuipatanisha mbingu na dunia ambayo imempokea na kumpatia fursa
ya kuishi kama binadamu katika mambo yote isipokuwa dhambi. Ni chachu ya upatanisho
kati ya mwanadamu na Muumba wake na kati ya binadamu na jirani yake.
Ameleta
mageuzi kwa wale waliokuwa wanadhaniana adui, waweze kujivika utu mpya na kuanza kushirikishana
kama marafiki na wenza katika hija ya maisha ya hapa duniani. Ikumbukwe kwamba, chuki,
uhasama, magomvi na vita ni kazi ya shetani, lakini waamini wa dini mbali mbali wanaweza
kushinda kishawishi hiki kwa kukumbatia misingi ya haki, amani,upendo na mshikamano
wa kidugu!