Waamini wasaidie mchakato wa binadamu kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani yake!
Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya kuleta mabadiliko katika Jamii, kwa njia
ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, katika ulimwengu huu ambao umekuwa kama
tambarabovu. Ili kukabiliana na changamoto zote hizi, Wakristo hawana budi kujishikamanisha
na Yesu Kristo, aliyekuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi
la dhambi na mauti, na hivyo, kumkirimia mabadiliko makubwa katika hija ya maisha
yake hapa duniani. Wakristo wanaweza kusaidia mchakato wa mwanadamu kujipatanisha
na Mungu pamoja na jirani yake.
Ni maneno ya Askofu mkuu Dr. Rowan Williams
wa Jimbo kuu la Cantebury, ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani,
wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli. Ili kuleta mabadiliko ya kweli, kuna haja
kwanza kwa waamini wenyewe kuchunguza dhamiri zao katika kioo cha ukweli na uwazi
mbele ya Mwenyezi Mungu; kwa kutambua na kuthamini wajibu na dhamana ambayo kila mwamini
amekabidhiwa na Jamii husika.
Wakristo wasikatishwe tamaa na magumu, changamoto
na kinzani mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika safari ya maisha yao hapa duniani.
Wajishikamanishe na watu wengine, wakitambua wajibu na dhamana yao ya kuwa ni chumvi
ya dunia na mwanga wa mataifa. Hii ndiyo changamoto kubwa inayoonesha ushupavu na
ushujaa wa kikristo unaojikita katika wito wa Kristo: tubuni na kuiamini Injili ili
muweze kubatizwa.
Maadhimisho haya ya Noeli kwa Mwaka 2012 yamekuwa ni ya mwisho
kwa Askofu mkuu Rowan Williams ambaye baada ya muda si mrefu atang’atuka kutoka madarakani
na kumwachia mrithi wake Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo Durham anayetarajiwa kusimikwa
rasmi hapo tarehe 21 Machi 2013.
Wakati wa mahubiri yake, Askofu mkuu Williams
amegusia kwamba, wajumbe wa mkutano mkuu wa Kanisa Anglikani uliohitimishwa hivi karibuni
wamekataa kuridhia pendekezo la kuwaweka wakfu wanawake ili kuwa Maaskofu wa Kanisa
Anglikani, jambo ambalo linaendelea kuwa ni kizingiti katika mchakato unaopania kudumisha
na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa Kanisa Anglikani na Wakristo
wengine katika ujumla wao.