Mwaka wa Imani uimarishe toba na wongofu wa ndani, ili kuchuchumilia utakatifu wa
maisha!
Maadhimisho wa Mwaka wa Imani ni changamoto na mwaliko kwa Familia ya Mungu sehemu
mbali mbali za dunia kujikita zaidi katika maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani,
kama kielelezo makini cha kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Wongofu wa ndani, unajikita
katika maisha ya sala. Ni changamoto inayotolewa na Askofu John Buckely wa Jimbo Katoliki
Cork na Ross nchini Ireland.
Familia ya
Mungu inaweza kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani kwa njia ya kujikita katika Tafakari
ya kina ya Neno la Mungu, linalomwilishwa katika uhasilia wa maisha ya waamini. Ni
mwaliko wa kujikita kusali kwa pamoja kwa kuanzia katika: Familia, Jumuiya Ndogo ndogo
na Vyama vya Kitume, kwa pamoja wakipania kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu,
linalowawezesha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Yesu
Kristo, muasisi wa Kanisa nyakati zote za historia ya Kanisa ameendelea kuibua watakatifu
na wafiadini kwa nyakati mbali mbali ili kuwa kweli ni kielelezo cha toba, wongofu
wa ndani na utakatifu wa maisha.
Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican ni mwaliko na changamoto ya kuchuchumilia toba na wongofu
wa ndani na kwamba, huu ni wito na mwaliko kwa kila mwamini na wale si kwa ajili ya
upendeleo wa watu wachache. Utakatifu upate chimbuko lake katika maisha ya sala na
imani tendaji, kwa kuomba ulinzi wa daima kutoka kwa Bikira Maria, Mwanamke wa Imani
aliyeonesha imani yake katika matendo kwa kuukubali Mpango wa Mungu katika maisha
yake, akawa tayari kuwashirikisha jirani zake, ile furaha ya kuwa Mama wa Mungu, Tabernakulo
ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.
Askofu John Buckley kutoka Ireland
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwashirikisha wengine ile furaha
ya kugundua tena imani yao, wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani; ili watu wengi
zaidi waweze kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Yesu Kristo; kwa kutekeleza dhamana
na wajibu waliojitwalia wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo.
Itakumbukwa
kwamba, Mwaka wa Imani uliozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita hapo tarehe 11 Oktoba 2012 utahitimishwa rasmi hapo tarehe 24 Novemba 2013, Katika
Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme.