Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Sinodi za Maaskofu wa Afrika na Katekisimu Mpya ya
ni sehemu ya hija ya imani katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani
Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni muhtasari makini wa Imani na mafundisho tanzu
ya maisha ya Kikristo ambayo ni utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na Mababa wa
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 50 iliyopita.
Ni sehemu
ya hija ya imani inayowachangamotisha waamini kusoma alama za nyakati, wakiwa tayari
kutekeleza mapenzi ya Mungu kadiri ya maisha na vipaumbele vyao.
Ni maneno
ya Mheshimiwa Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika la Waconsolata, katika
mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu viashilia vya imani kama sehemu ya maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, unaowachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanaifahamu vyema
imani yao, ili waweze kukua, kukomaa na kuimarisha, kiasi hata cha kutoka kifua mbele
kuishuhudia kwa njia matendo adilifu.
Hija ya imani anasema Padre Pendawazima,
inajionesha pia katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu Bara la Afrika yaliyokazia
kwa namna ya pekee umuhimu wa Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa uenezaji wa
Injili hadi miisho ya dunia. Maadhimisho ya Sinodi ilikuwa ni alama ya mshikamano
wa kiimani miongoni mwa Familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika.
Maadhimisho
ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika baada ya miaka kumi na tano tangu
ilipoadhimishwa ile Sinodi ya kwanza iliyoletwa mwamko na ari mpya ya maisha na utume
wa Kanisa Barani Afrika, kwa wakati huu, waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo vya
upatanisho, haki, amani na msamaha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna dalili
nyingi zinazoonesha hali tete ya imani, amani, matumaini na mapendo miongoni mwa Familia
ya Mungu Barani Afrika. Changamoto zote hizi zinapaswa kufanyiwa kazi kama sehemu
ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.