Kuna magenge ya vijana wasiokuwa na fursa za ajira Zanzibar yanatumiwa kuhujumu misingi
ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa Visiwani Zanzibar!
Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu
ya Noeli, amezungumzia tatizo la kukithiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya
inayosababisha madhara makubwa kwa Jamii visiwani Zanzibar na kwamba, umefika wakati
kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwafichua na hatimaye, kuwachukulia hatua za kisheria.
Serikali iwavalie njuga wafanyabiashara wakubwa ili kukata mzizi wa biashara hii haramu
inayoendelea kusababisha madhara makubwa kwa wananchi Zanzibar.
Jamii iwajibike
kuwasaidia wathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ambao wanajikuta wametumbukia
huko kutokana na umaskini pamoja na sababu mbali mbali za maisha. Kuna kundi kubwa
la vijana Visiwani Zanzibar ambalo halina fursa za ajira, linaishi katika mazingira
hatarishi na matokeo yake ni kujitumbukiza katika matumizi haramu ya dawa za kulevya
na ukahaba; mambo ambayo pia yanachangia kuongezeka kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
na makosa ya jinai.
Kundi hili limeanza kutumiwa na baadhi ya wanasiasa na
viongozi wa kidini wanaotumia vijana hawa wasiokuwa na ajira kwa malengo binafsi.
Ghasia na uchomaji wa Makanisa Visiwani Zanzibar chini ya mwamvuli wa kupinga muungano
ni dhana nyemelezi ya wenye madaraka nje na ndani ya Visiwa vya Zanzibar kutaka kutumia
umaskini wa vijana kuhataraisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Askofu Shao
anawahimiza vijana kukataa katu katu kutumiwa kwa misingi ya dini, itikadi za kisiasa
na kiuchumi kwa manufaa ya watu binafsi.
Wananchi wanatakiwa kutoa maoni yao
kuhusu Katiba Mpya itakaozingatia mafao ya wengi, uhuru wa kuabudu pamoja na kudumisha
misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Wakati huo huo habari
kutoka Zanzibar zinabainisha kwamba, Jeshi la Polisi limewatia watu wawili mbaroni
kwa kuhusishwa na tuhuma za kumshambulia kwa risasi Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo
Katoliki Zanzibar. Watu hao wanaendelea kuhojiwa na Polisi ili kuwapata watu wengine
walioshiriki katika kupanga na kutekeleza njama ya kuvamia na kumjeruhi Padre Mkenda
kwa risasi, tukio ambalo limevuta hisia kubwa ndani na nje ya Tanzania. Inasemekana
kuna genge la watu ambalo limekuwa likifanya hujuma dhidi ya viongozi wa kidini na
watu wasiokuwa na hatia Visiwani Zanzibar wanaosimama kidete kutangaza haki, amani,
upendo na mshikamano wa kitaifa.
Padre Ambrose Mkenda mwenye umri wa miaka
hamsini na mbili, Paroko wa Parokia ya Mpendae amekuwepo Zanzibar tangu mwaka 1995
na ameendelea na utume wake bila shida wala wasi wasi. Anasema, kuna haja sasa kwa
Serikali kuchukua hatua kali zaidi kwa watu wanaochezea na kutaka kuhatarisha misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa Visiwani Zanzibar. Hii ni dhamana
inayopaswa kufanyiwa kazi ndani ya Familia na Jamii katika ujumla wake, ili kupata
kizazi cha watu wanaoheshimihana na kuthaminiana kamka ndugu.
Takwimu zinaonesha
kwamba, kuanzia mwaka 2001 hadi kufikia mwaka 2012 jumla ya Makanisa 25 pamoja na
baa 12 zilichomwa moto na "watu wasiojulikana". Hadi sasa hakuna taarifa rasmi zinazoonesha
kwamba, watu hawa wametiwa mbaroni na wanatakiwa kujibu tuhuma zinazowakabili.
Padre
Ambrose Mkenda alipigwa risasi shingoni tarehe 25 Desemba 2012 majira ya saa 1: 45
katika eneo la Tomondo. Akafanyiwa operesheni ili kuondoa risasi zilizokuwa mwilini
mwake hapo Ijumaa tarehe 28 Desemba 2012, kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tangu wakati huo viongozi waandamizi kutoka Serikalini wamemtembelea Padre
Mkenda ili kumtakia hali. Kati yao ni Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,Makamu wa Rais Dr. Mohammed Gharib Bilal; Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohammed. Rais mstaafu wa
awamu ya tatu, Benjamini William Mkapa naye amemtembelea Padre Ambrose Mkenda. Wapenda
haki na amani wanafuatlia kwa umakini mkubwa mkasa huu ambao umeibua hisia tofauti
kuhusu haki, amani na mshikamano wa kitaifa Visiwani Zanzibar.