Jukumu la Familia kama Kanisa Dogo la Nyumbani katika Uinjilishaji Mpya!
Ndugu msilizaji wa Radio Vatican tunayo furaha kubwa leo kutafakari kwa pamoja Maadhimisho
ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu katika mwaka huu wa imani.
Mwaka unaotawaliwa na wazo la uenjilishaji mpya. Wazo la uenjilishaji mpya ni utume
wa kanisa ambao unapata chimbuko lake kwa Kristo mwenyewe (Matayo 28: 19-20). Mwenyeheri Yohane
Paulo wa pili alipolitaja wazo la Uinjilishaji mpya mwaka 1983 alikiri kuwa ni wazo
lililopevuka katika maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaotimiza miaka
50 ya uwepo wake na kupata msukumo mkubwa katika hati ya kichungaji ya papa Paulo
VI Evangelii Nuntiandi yaani Uinjilishaji katika Ulimwengu mamboleo wa mwaka 1975.
Ni Uinjilishaji uleule Kristo alioufanya na alioamuru kanisa lake kuufanya kwa
nyakati zote lakini unakuwa uenjilishaji mpya kwani ufanyike kwenye mazingira ya wakati
wetu wenye makandokando yake na namna yake ya kufikiri na kutenda. Kama ni utume
wa kanisa basi basi ni utume wa Familia iliyo Kanisa dogo la nyumbani ambalo mfano
wake ni wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu tunayoishangilia kwa namna ya
pekee leo. Familia hii haikurudi nyuma kati ujenzi wa jumuiya ya kibinadamu, katika
uzazi na malezi na ndilo Fumbo la Mungu kuwa mtu tunaloadhimisha wakati wa Siku kuu
ya Noeli, Katika mahusiano na jamii pamoja na Mungu mwenyewe. Kumbe mifano tuyoipata
hapo inatuhakikishia kuwa Familia ni chimbuko la uenjilishaji mpya kwani Familia iliyo
Kanisa dogo la nyumbani ndiye Muinjilishaji namba moja ndiyo maana hata Mtoto Yesu
alipata nafasi ya kushikishwa katika mambo yote ya kiibada waliyofwata wazazi wake
na akaongezeka katika kimo na hekima (Lk 2: 52). Pia Familia ni kilele cha Uinjilishaji
kwani wakati wote familia takatifu ilijifunza kupokea na kutekeleza maagizo ya Mwenyezi
Mungu. Ndugu msilizaji, katika tafakari yetu ya mwaka huu wa imani ni vizuri tujipime
kuwa ni kwa kiasi gani Familia yetu imebaki kuwa jumuiya inayoamini na enjilisha ndani
na nje ya familia yetu? Ni kwa kiasi gani Familia yetu imeendelea kuwa chombo cha
Sala na Liturujia ya Kanisa? Ni kiasi gani Familia yetu imeendelea kuwa chombo cha
huduma kwa Mungu na kwa mwanadamu mwingine? Hatujachelewa kufanya mabadilko ndio
maana tumepata nafasi ya kuadhimisha sherehe hii ya familia takatifu katika mwaka
huu wa imani na uenjilishaji mpya ili tujipange tena. Tukiwa na nia njema kwa maombezi
ya familia takatifu tutafika. Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi padre Raphael
Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa
Laterano- Roma.