2012-12-31 09:46:01

Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano wa kuigwa katika: Imani, upendo, heshima na Ibada ya kweli!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Jumapili tarehe 30 Desemba 2012, alisema kwamba; Liturujia ya Neno la Mungu inawaonesha Bikira Maria na Yosefu wakipanda kwenda Yerusalem kama ilivyokuwa desturi wakati wa Siku kuu ya Pasaka, wakiwa na Mtoto Yesu aliyekuwa na umri wa miaka kumi na miwili.

Mara ya kwanza kwa Yesu kuingia Hekaluni, ilikuwa ni siku arobaini mara baada kuzaliwa kwake, wazazi walipokwenda kutolea sadaka ya maskini, kama anavyosimulia Mwinjili Luka ambaye amejikita katika taalimungu ya umaskini kwa kuwakumbatia maskini.

Anasema, Familia Takatifu ilihesabiwa kuwa ni kati ya Familia Maskini. Wakati huu Yesu yuko Hekaluni akiwa na dhamana tofauti kabisa, akiwa mstari wa mbele, jambo linalowashirikisha pia Maria na Yosefu, kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria. Ni Familia iliyonesha moyo wa Ibada.

Bikira Maria na Yosefu wanaporudi nyumbani, Mtoto Yesu anajikuta amebaki Hekaluni, jambo lililopelekea wazazi hawa kumtafuta kwa siku tatu na hatimaye, wanamkuta Hekaluni akijibizana na walimu wa sheria, kwani hapa ni mahali pake, ni nyumbani mwa Baba yake ambaye ni Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Yesu Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, wasi wasi na woga waliokuwa nao Bikira Maria na Yosefu ni jambo la kawaida kwa wazazi wanaomwelimisha mtoto wao na kumwingiza katika maisha ili hatimaye, aweze kutambua ukweli wenyewe. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kusali kwa ajili ya kuombea Familia mbali mbali duniani, ili kwa njia ya mfano wa Familia Takatifu ya Nazareti, wazazi na walezi waweze kujitoa kikamilifu kwa ajili ya makuzi na elimu ya watoto wao bila kusahau kuwarithisha imani ambayo ni zawadi muhimu sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomwilishwa pia kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali ili kwamba, kila mtoto anayezaliwa aweze kupokelewa kama zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye kuonjeshwa upendo kutoka kwa wazazi wake, ili aweze kukua na kukomaa katika hekima na akili mbele ya Mwenyezi Mungu na wanawadamu. Upendo na uaminifu wa Familia Takatifu uwe ni mfano na kielelezo cha kuigwa na wanandoa wote wa Kikristo, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa maisha.

Ukimya wa Mtakatifu Yosefu mtu wa haki na mfano wa Bikira Maria aliyekuwa anahifadhi yote moyoni mwake ni mwaliko wa kutoa nafasi kwa imani ya Familia Takatifu kuweza kupenya katika maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anazitakia Familia za Kikristo maisha yanayotambua uwepo wa Mungu, wakichuchumilia upendo na furaha kama ilivyotawala katika maisha ya Bikira Maria na Yosefu.

Ziwe ni familia ambazo zinaonesha imani, upendo, maelewano, heshima na ibada ya kweli. Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote kheri na baraka kwa Mwaka Mpya wa 2013, wakitembea katika Mwanga na Amani ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.