Askofu mkuu Rugambwa aanza ziara ya kichungaji nchini Siera Leone
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa
watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kuanzia tarehe 31 Desemba 2012
hadi tarehe 7 Januari 2013 atakuwa na ziara ya kichungaji nchini Siera Leone ili kumweka
wakfu na hatimaye kumsimika Askofu mteule Henry Aruna wa Jimbo Katoliki Makeni.
Askofu
mkuu Rugambwa, akiwa nchini Siera Leone, hapo tarehe 5 Januari 2013 anatarajiwa kukutana
na Baraza la Maaskofu Katoliki Siera Leone pamoja na Makleri wa Jimbo Katoliki Makeni.
Atatembelea Seminari kuu Mtakatifu Paulo iliyoko Mjini Freetown pamoja na kukagua
miradi inayofadhiliwa na Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.
Kwa takribani
miaka ishirini na mitano, Jimbo Katoliki Makeni liliongozwa na Askofu George Biguzzi.
Takwimu zinaonesha kwamba, waamini wa Jimbo Katoliki Makeni ni zaidi ya 50, 000, sehemu
kubwa ya wakazi wa Makeni ni waamini wa dini ya Kiislam. Jimbo lina jumla ya Parokia
kumi na mbili zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 32 na Mapadre wa Mashirika ya kitawa
ni 34. Kuna Mapadre wa Fidei Donum 4. Jimbo lina jumla ya Makatekista 156. Lina taasisi
za elimu katika ngazi mbali mbali zipatazo 219 na taasisi za huduma ni 9.
Askofu
mteule Henry Aruna wa Jimbo Katoliki Makeni alizaliwa tarehe 2 Agosti 1964. Akapadrishwa
tarehe 16 Aprili 1992. Tarehe 7 Januari 2012, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, akamteua kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Makeni, Siera Leone.