Wanyama watunzwe, lakini binadamu apewe kipaumbele cha kwanza!
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anawataka wananchi wa Afrika ya Kusini kudumisha
utu na heshima ya binadamu ndani ya familia badala ya kutumia nguvu na rasilimali
nyingi kwa ajili ya kujenga urafiki na mbwa, kwamba, kimsingi huu si utamaduni wa
mwafrika. Bara la Afrika lina mila na tamaduni njema ambazo zinapaswa kupewa kipaumbele
cha pekee kuliko kuiga mambo hata yale ambayo hayana maana sana kwa maisha ya Watu
wa Afrika.
Maneno haya ya Rais Zuma yameibua mjadala mzito miongoni mwa wanaharakati
na watetezi wa haki za wanyama waliojitokeza katika mitandao ya kijamii kupinga msimamo
wa Rais Zuma. Kuna mamillioni ya watu ambao wanakabiliwa na baa la umaskini nchini
Afrika ya Kusini, kumbe, kuna mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa nchi.
Watu
wajifunze kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu, kwani pale mtu anapohamisha upendo
wake kutoka kwa mwanadamu na kuelekeza kwa mnyama, kuna kasoro kubwa anasema Rais
Zuma. Wanyama watunzwe, lakini mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza, ndio ujumbe
ambao Rais Jaco Zuma alitaka kuufikisha kwa wananchi wa Afrika ya Kusini.