Padre Mkenda kufanyiwa Operesheni, Serikali Zanzibar yaahidi kuwasaka wahusika ili
sheria iweze kushika mkondo wake!
Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo Katoliki Zanzibar aliyepigwa risasi hivi karibuni anatarajiwa
kufanyiwa operesheni kubwa, Ijumaa tarehe 28 Desemba 2012, ili kuondoa risasi mbili
zilizoko mwilini mwake na kwamba, amevunjika taya, lakini anaendelea vyema, kadiri
ya taarifa kutoka katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Madaktari
wamekuwa wanaendelea na juhudi za kurekebisha taya lililovunjika baada ya Padre Ambrose
Mkenda kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika mkesha wa Siku kuu ya Noeli, katika
eneo la Tomondo, nje kidogo ya mji wa Unguja, tukio ambalo limewasikitisha wapenda
amani ndani na nje ya Tanzania.
Serikali ya Mapinzduzi Zanzibar imeahidi kutenda
haki kwa kuhakikisha kwamba, watuhumiwa wanapatikana na kufikishwa kwenye mkondo wa
sheria ili kujibu mashtaka. Hadi kufikia Ijumaa, tarehe 28 Desemba, 2012 hakuna mtu
aliyekuwa amekwishakamata kuhusiana na tukio hili ambalo bado linaendelea kuacha maswali
mengi yasiyokuwa na majibu! Hili ni tukio la pili kwa kutendwa dhidi ya viongozi wa
kidini kwa siku za hivi karibuni Visiwani Zanzibar.