2012-12-27 11:01:47

Hali ya Padre Ambrose Mkenda aliyepigwa risasi Zanzibar, bado ni tete!


Jeshi la Polisi Zanzibar linaendelea kufanya uchaguzi kuhusu tukio la Padre Ambrose Mkenda wa Jimbo Katoliki Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwenye kesha la Siku kuu ya Noeli na hivyo kumsababishia majeraha makubwa mdomoni na shingoni, hali iliyopelekea Padre Mkenda kupoteza damu nyingi.

Kutokana na hali yake kuwa mbaya, ilibidi apelekwe kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili Dar Es Salaam kwa matibabu zaidi. Wadadizi wa mambo wanasema pengine watu walifanya tukio hili la kinyama walikuwa wanataka kupora sadaka ya Kesha la Noeli.

Jukwaa la Wakristo Tanzania, katika ujumbe wake wa Noeli kwa Watanzania na watu wenye mapenzi mema, limeonya kuhusu kuteteleka kwa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kutokana na chuki za kidini, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi mapema sana kabla taifa halijatumbukia kwenye maafa makubwa.

Padre Ambrose Mkenda ni Paroko wa Parokia ya Mpendae, Jimbo Katoliki Zanzibar. Askofu Agustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar amenukuriwa akisema kwamba, hadi sasa Jimbo halina taarifa ya watu waliohusika na tukio hili na kwamba, Jeshi la Polisi Zanzibar bado linaendelea na uchunguzi.







All the contents on this site are copyrighted ©.