2012-12-27 08:35:03

Familia ni kitovu cha utume wa Kanisa katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba familia ni kitovu cha utume wa Kanisa katika Uinjilishaji Mpya. Kwa kuinjilisha familia, Jamii nzima itakuwa imeinjilishwa. Hayo yamesemwa na Askofu Hilary Okeke wa Jimbo Katoliki la Nnewi, Nigeria, wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Wanasheria za Kanisa nchini Nigeria, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “ Shughuli za kichungaji kwa ajili ya Familia: utume na changamoto zake. RealAudioMP3

Familia ni kati ya taasisi ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ndoa na familia za Kikristo zinapaswa kusimama kidete, vinginevyo zinaweza kumezwa na malimwengu kutokana na Jamii kukengeuka. Uinjilishaji Mpya hauna budi kufanyika kwa kutoa kipaumbele kwa Familia ambayo ni urithi wa kila mwanadamu na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.

Hapa ni mahali ambapo wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusamehewa; kupokea na kutoa kwa njia ya ukarimu. Familia ni shule ya kwanza kabisa inayorithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Watoto wana uwezo wa kupokea kile kinachotolewa na wazazi pamoja na walezi wao, kumbe, wazazi na walezi wanapaswa kuwa kweli ni mifano bora ya kuigwa kwa maneno na matendo yao!

Askofu Okeke anawaalika Wanasheria wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha utakatifu na tunu msingi za maisha ya kifamilia mintarafu Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia.

Wajumbe wa mkutano huu wamekazia umuhimu wa mafunzo ya awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa, ili waweze kutambua na kuthamini ndoa ya Kikristo ambayo ni ya kudumu hadi kifo kitakapowatenganisha kadiri ya mpango wa Mungu. Wanandoa watarajiwa waepukane na uchumba sugu unaowanyima kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Okeke alionesha masikitiko yake kutokana na athari zinazojitokeza kwenye ndoa za wake wengi, zinazoendelea kumdhalilisha mwanamke na kumfanya kuwa ni chombo tu cha kukidhi tamaa ya mwili. Kanisa Barani Afrika halina budi kujitahidi kuhakikisha kwamba, linaonesha uzuri wa maisha ya ndoa na familia kwa kuzingatia mila na desturi nzuri za Kiafrika.

Watu hawana budi kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, ili kukuza na kudumisha upendo wa dhati; umoja na mshikamano; amani na utulivu. Wanawake waheshimiwe na kuthaminiwa utu na nafasi yao katika maisha ya ndoa na familia na wala si vichokoo vya kukidhi matamanio ya wanaume. Ndoa za wake wengi ni kielelezo cha unyanyasaji wa kijinsia, dhuluma, kinzani na migawanyiko, kinyume kabisa na utamaduni wa upendo wa dhati ambao Mwenyezi Mungu aliudhamiria kwa ajili ya mwanadamu tangu kuumbwa kwake na Kristo akautakatifuza kwa kuweka Sakramenti ya ndoa kati ya Bwana na Bibi.

Uhuru usiokuwa na mipaka na watu kupenda kujitawala bila kuwajibika, kumepelekea ongezeko kubwa la talaka na baadhi ya watu kukumbatia utamaduni wa kuenzi “vidumu” au nyumba ndogo kama zinavyojulikana kwa Waswahili wengi.

Lakini jambo la kushangaza ni kule kukengeuka kwa watu kimaadili kiasi kwamba, watu wa jinsia moja wanataka kufunga ndoa, jambo ambalo linapigiwa debe na baadhi ya nchi za Magharibi, kiasi hata cha kutishia kuchomoa misaada kwa nchi zile ambazo hazitaridhia sheria eti kama kielelezo cha uhuru na haki sawa. Huu ni utamaduni wa kifo unaosigana na mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji.

Kanisa lazima lisimame kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kuheshimu na kutunza mila na tamaduni njema za kiafrika badala ya kugenishwa na mambo yanayopelekea kumong’onyoka kwa maadili na utu wema. Ndoa ya Kikristo inajengeka katika msingi wa Bwana na Bibi, wakipania kupata watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni agano la kudumu kati ya watu wawili wanaopendana na kushibana kwa dhati bila shuruti.

Kanisa kwa njia ya Katekesi ya kina, Sheria na Kanuni za maisha ya ndoa linapenda kulinda na kutunza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ni dhamana kwa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaonesha utakatifu wa maisha katika ndoa na wala si tendo la watu kuishi kwa pamoja tu! Hii ni Sakramenti, chemchemi ya neema na utakaso, inayowawezesha wanandoa kusaidiana katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili hatimaye, kufikia utakatifu.

Familia haina budi kuwa ni shule ya kwanza ya tunu msingi za kiroho na maisha adili; ioneshe utakatifu wa maisha mintarafu upendo wa Kristo kwa Kanisa lake. Waamini wachangamotishwe kupenda na kuthamini tunu msingi za maisha ya ndoa na familia za Kikristo, kamwe wasimezwe na malimwengu, huko watapotea!








All the contents on this site are copyrighted ©.