Familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia!
Mara nyingi ninapotafakari neno familia mawazo yangu yanavutwa kutafakari mfano wa
Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Tunapotafari kuhusu familia tuyapeleke
mawazo yetu kwa baba, mama na watoto kama ilivyokuwa katika Familia Takatifu ya Yesu,
Maria na Yosefu.
Familia Takatifu
inatukumbusha mwaliko wetu wa kuwa watakatifu; na familia inapewa heshima kubwa ya
kuwa ni shule ya kwanza ya utakatifu. Tukitafakari Fumbo la Mungu kujifanya mwanadamu,
tunaweza kujiuliza maswali mengi na swali mojawapo ni kwanini Mungu aliamua kushuka
kwetu kwa kupitia njia ya familia? Kutokana na uwezo wake angeweza kuja kwa njia nyingine
yeyote ambayo angependelea.
Lakini, mpango wa Mungu kujifanya mtu kwa uwezo
wa Roho Mtakatifu, kuzaliwa kama binadumu wa hali ya chini na kuishi kama sisi binadamu
akiwa sawa katika mambo yote isipokuwa dhambi, ni kutualika sisi wote tuweze kuwa
kama yeye, maana yake tuweze kuwa watakatifu na utakatifu huo anatuonesha kuwa unaanzia
katika familia zetu.
Bwana wetu Yesu Kristo anatuonesha njia pekee yenye kuleta
mafanikio katika maisha ya familia ni: unyenyekevu kwa Mungu na kunyenyekeana wenyewe
kwa wenyewe. Kristo na Umungu wake alijinyenyekesha na kuzaliwa na Bikira Maria, akawa
ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu. Bikira Maria na Yosefu walikuwa wanyenyekevu
kupokea mapenzi ya Mungu katika maisha yao na pia walinyenyekeana wao kwa wao.
Bila
mume na mke kuwa wanyenyekevu kwa Mungu yaani kupokea Neno la Mungu na kufuata maongozi
yake kupitia Kanisa lake takatifu, na bila mume kuwa mnenyekevu kwa mke na mke kuwa
mnyenyekevu kwa mume katika kutimza dhamana na majukumu ya kila siku familia hawezi
kusimama imara.
Mume na mke wanapoamua kuishi pamoja kama mume na mke wanapokea
mwaliko wa kuwa watakatifu na kuwasaidia watoto watakaojaliwa kama zawadi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu kuupata utakatifu. Kazi ya kwanza ni kusaidiana wenyewe kama mume na
mke kuwa watakatifu; kazi ya pili ni kuwasaidia watoto wao kuwa watakatifu na kazi
ya tatu ni kuwa mwanga na chumvi kwa taifa zima la Mungu kwa mifano bora na tunu msingi
za maisha ya kifamilia.
Katika ulimwengu wetu, kuna mambo mengi ambayo yanaweza
kuhatarisha zawadi kubwa ya maisha ya familia. Kwa leo ningependa tutafakari pamoja
changamoto moja kuhusu tatizo la uchumba sugu katika jamii zetu. Ninapozungumzia uchumba
sugu: ninamaanisha mume na mke kuamua kuishi pamoja kwa muda mrefu bila kuomba Baraka
za Mungu katika Sakramenti ya Ndoa. Matokeo yake tunashindwa kuweka mahusiano yetu
wazi mbele ya Mungu na taifa zima la Mungu, na kumwomba Mwenyezi Mungu abariki uhusiano
huo na kutujalia neema ya kuishi agano tunalo mwahidia katika msingi wa Ndoa Takatifu.
Mara nyingi “wapenzi wawili” wanapokutana na kutaka kuishi pamoja wanatumia
neno upendo “ninakupenda”, lakini wakisha amua kushi pamoja wanasema kwamba “tunapimana”.
Kama tunasubiri mpaka tuwe watakatifu ndipo tuweze kuweka agano la ndoa hali hiyo
haiwezekani katika ulimwengu huu. Maisha ya kutafuta utakatifu ni mapambano ya kila
siku katika maisha yetu.
Neno linalotumika mwanzoni watu wanavyoanza kutafutana
“ninakupenda”, katika lugha ya kibinadamu ni sawasawa kwasababu mara nyingi binadamu
tunatawaliwa na vionjo, lakini, neno hilo linahitaji kukamilishwa na upendo wa Kimungu.
Hivyo basi hii hali ya vionjo vya kibinadamu katika kupenda inapokamilishwa na upendo
wa kimungu inatengeneza mapendo ya kweli kati ya mume na mke. Mtu hawezi kuwa na upendo
wa kimungu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu kama hajajaliwa na Mungu mwenyewe.
Zawadi
ya upendo wa Kimungu tunajaliwa tunapokuwa na ushirikiano mzuri na Mungu katika maisha
yetu ya kila siku, yaani Kusoma na kutafari Neno la Mungu mara kwa mara katika maisha
yetu na kuwa tayari kupokea wajibu tunaopewa na Neno hilo; kushiriki kiaminifu katika
Sakramenti za Kanisa hususani Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu; kuishi maisha
ya Sala na kumkabidhi Mungu awe kiongozi mkuu wa maisha yetu.
Dalili ya upendo
wa Kimungu katika familia inadhihirishwa na mtu kujitoa kwa mwenzake kama alivyo na
kumpokea mwenzake kama alivyo; yaani: katika mazuri na mapungufu, na kusaidiana kwa
pamoja kwa msaada wa Mungu kuboresha yale mazuri na kurekebisha yale mapungufu; maana
yake: kusaidiana katikaka kuutafuta utakatifu.
Sote tunaalikwa kutafuta utakatifu
kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Yesu mwenyewe anatueleza wazi ya kuwa “mtu
yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake wa kila siku,
anifuate”(LK 9:23). Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba,
utakatifu ni wito na mwaliko kwa kila mfuasi wa Kristo na wala si fursa kwa watu wachache
ndani ya Kanisa, kama alivyokazia Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta. Kutoka Studio
za Radio Vatican, mimi ni Shemasi Titus Nkane, OSB.