2012-12-26 09:57:58

Wekezeni katika elimu kama njia ya kumkomboa mwanadamu: kiroho na kimwili!


Askofu Godrey Mdimi Mhogolo wa Kanisa Anglikani, Dayosisi ya Kati, anawataka watanzania kuenzi Fumbo la Umwilisho kwa kuwekeza katika sekta ya elimu ambayo ni dira na msingi wa maendeleo ya mtu kiroho na kimwili. Kuna umuhimu wa kujenga na kuimarisha msingi wa elimu bora kwa ajili ya maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; sanjari na mapambano dhidi ya baa la umaskini unaowakabili Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Askofu Mhogolo ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Roho Mtakatifu, Dodoma. Kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, kunapania kumletea mwanadamu ukombozi wa kweli kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni changamoto kwa watanzania kujifunga kibwebwe kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.

Ni jukumu lao kulinda, kutetea na kudumisha amani kwa njia ya elimu inayojikita katika: upendo, mshikamano, ukweli, msamaha na upatanisho. Toba na wongofu wa ndani iwasaidie watanzania kuondokana na mambo yanayosigana na maadili na utu wema kama vile: rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Kutokana na watu kutafuta mali kwa nguvu sana, wanajikuta wakipokonya haki msingi za watu wengine ndani ya Jamii, jambo ambalo ni hatari sana.

Wakristo wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza katika sekta ya elimu nchini Tanzania, kwani kati ya Vyuo 19 vilivyoko nchini Tanzania, vyuo 7 vinamilikiwa na kuendeshwa na Wakristo, Vyuo 11 vinamilikiwa na Serikali na Waamini wa dini ya Kiislam Tanzania wanaendesha chuo kikuu kimoja! Dodoma imeaanza kubadilika na kuboreka kutokana na uwepo wa Vyuo vikuu na taasisi nyingi za elimu ya juu.

Anawataka wananchi wa Dodoma kutokatishwa tamaa na hali ya hewa na historia iliyokuwepo tangu awali, kwani Mungu amemkirimia mwanadamu akili na ufahamu, ana uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yake. Ni changamoto ya kujipanga upya, kwani kila jambo linawezekana kwa msaada wa Mungu.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Amani Karume ni kati ya watanzania wanaopaswa kuendelea kuenziwa kutokana na mchango wao mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote; ni kielelezo cha: uhuru, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa; walikuwa ni kimbilio la watu waliokuwa na shida kutoka ndani na nje ya Tanzania. Viongozi hawa ni mfano bora wa kuigwa na Jamii ya watanzania, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.