Wasomi jengeni uhusiano mwema na Yesu Kristo muweze kufahamu maana na hatimaye, kufurahia
maisha!
Yesu Kristo ndiye Mkombozi pekee wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Anahitaji kukutana na wasomi ili kuwaonesha maana halisi ya maisha na furaha ya kweli
inayobubujika kutokana kwake.
Hii ni changamoto
kwa wasomi kujitahidi kumjifunza na kumwelewa Yesu Kristo na hatimaye, kujenga uhusiano
wa dhati pamoja naye kwa njia ya: maisha ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti
za Kanisa pamoja na Matendo ya huruma.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa
Mwaka 2012 kutoka kwa Mheshimiwa Padre Charles Kitima, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT kwa wasomi na wanazuoni sehemu mbali mbali
za dunia. Anawaalika wasomi hao kumjifunza Yesu Kristo kisayansi, kwa kutoa nafasi
katika maisha na vipaumbele vyao, hapo watakuwa na fursa kubwa ya kufahamu maana ya
maisha, utu, heshima na hatima ya binadamu kwa siku za usoni.
Padre Charles
Kitima katika mahojiano maalum na Radio Vatican anawaambia wasomi na wanazuoni kwamba,
wakibobema katika haya, kwa hakika watakuwa na furaha ya kweli katika maisha yao!
Mengine yote yanapita, lakini Kristo ni yule yule, Jana, Leo na Hata Milele, Yeye
ni Omega, Mwanzo na Mwisho; nyakati zote ni zake.