2012-12-25 10:39:23

Yesu Kristo ni Mtu kweli na Mungu kweli: hiki ni kiini cha Imani ya Kanisa


Noeli ya Mwaka 2012 ni kielele cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na baraka ambazo amelikirimia Kanisa kwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama fursa ya kutangaza Imani ya Kikristo pamoja na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. RealAudioMP3

Hii ni changamoto ya kumpenda na kumshuhudia kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya watu kwake kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo.

Ni matashi mema kutoka kwa Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha, Tanzania katika Siku kuu ya Noeli sanjari na mwendelezo wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Anasema, Noeli ni Siku kuu ya Fumbo la Umwilisho, linaonesha kwa namna ya pekee, upendo na unyenyekevu wa Mungu kwa kumtoa Mwanaye wa Pekee Yesu Kristo kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo ni Mtu kweli na Mungu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, ni Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba.

Kipindi cha Noeli, iwe ni fursa ya kuimarisha Imani kwa Kristo: Mtu kweli na Mungu kweli, ili aweze kuzaliwa tena katika uhalisia wa maisha ya kila mwamini, sanjari na kumpatia nafasi na kipaumbele cha kwanza, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni Rafiki na mdau mkuu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano.

Yesu Kristo ni Mtu kweli na Mungu kweli, ndicho kiini cha Imani ya Kikristo ambayo mwamini anaipokea kutoka ndani ya Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Askofu mkuu Lebulu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kuhakikisha kuwa wanatumia vyema maadhimisho mbali mbali yaliyopangwa katika Mwaka wa Imani, ili kuifahamu, kuiadhimisha, kuishuhudia na kuwashirikisha wengine furaha kuu ya Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hadi pale watakapoungana na Mwenyezi Mungu kufurahia uzima wa milele.







All the contents on this site are copyrighted ©.