2012-12-25 10:19:43

Hati za Papa kuhusu watakatifu na wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa hivi karibuni


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameruhusu Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kuchapisha hati inayotambua fadhila za kishujaa za Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa sita. Baba Mtakatifu ametoa ruhusa hii alipokutana na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza hilo la Kipapa hivi karibuni. RealAudioMP3

Hati hii inafungua njia kwa Papa Paulo wa sita kuweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri. Baba Mtakatifu pia ametia sahihi nyaraka nyingine ishirini na tatu. Ametambua miujiza iliyotendwa kwa maombezi ya wenyeheri wafia dini kutoka Jimbo Katoliki la Otranto, walioyamimina maisha yao kwa kumuungama Kristo kunako mwaka 1480. Wengine ni watawa wawili waanzilishi wa Mashirika Laura wa Mtakatifu Katarina wa Siena (1874 – 1949 pamoja na Maria wa Guadalupe (1878 – 1963.

Kuna Watumishi wa Mungu watano: Askofu Antonio Franco (1585 – 1626), Padre Giuseppe Gabriele wa Rozari Brochero kutoka Argentina (1840 – 1914), Mwanzilishi wa Shirika Padre Cristoforo di Santa Cristina (1638- 1690). Wengine ni watawa wawili waanzilishi wa Mashirika nao ni: Sofia Czeska Maciejowska (1584 – 1650) kutoka Poland; Marherita Lucia Szewczyk (1828 – 1905) kutoka Ucrain.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ametambua pia ushujaa ulioneshwa na Padre mmoja kutoka Croatia aliyeuwawa kinyama kunako mwaka 1947 kutokana na chuki za kidini, bila kuwasahau watawa wa kiume na kike waliouwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake nchini Hispania kati ya Mwaka 1936 hadi mwaka 1938.

Mwishoni, Baba Mtakatifu ameruhusu pia kuchapishwa hati inayotambua fadhila za kishujaa za watumishi wa Mungu kumi, kati yao kuna Papa Paulo wa sita; kuna Askofu mmoja, Mapadre wawili na watawa sita.








All the contents on this site are copyrighted ©.