Siku kuu ya Noeli itusaidie kutafakari kuhus: Imani, Matumaini na Mapendo ya Mungu
kwa binadamu!
Waamini wapenzi, Tumsifu Yesu Kristo!
Ndugu zangu
ni Noeli. Fumbo kuu la Noeli liko katika maneno haya“Neno akatwaa mwili na kujenga
hema yake kati yetu!” Sikukuu ya leo ni kilele cha tafakari ya Kanisa juu ya fumbo
hilo la Noeli.
Noeli, ni sikukuu inayojulikana sana ulimwengu, na karibu imechukua
sura ya kiutamaduni zaidi kuliko ile ya kikristu. Siku ya noeli imekuwa ni sikukuu
ya kujimwaga kwenye maraharaha na hasa kwenye uchumi. Sisi tunaosadiki bado katika
mtoto huyu aliyezaliwa maskini na kwenye mazingira ya kimaskini, leo tunaalikwa kumkaribisha
mioyoni mwetu, aweze kupata makao, kumbembeleza, kumshangaa, kumfurahia na kumwabudu.
Tuwe na imani hai, matumaini halisi, na upendo mkubwa wa kuweza kumkaribisha
Yesu anayekuja. Tuingine katika fumbo la Noeli kwa hisia ya imani, matumaini na upendo
ili mioyo yetu iweze kupanuka na kumwachia nafasi kubwa ya kuingia mtoto anayefika,
pasipo sisi kuchanganyikiwa na mianga mingine ya uwongo na sauti danganyifu za ulimwengu
wetu wa leo.
1. Kuwa na imani:
Tunatambua kwamba katika mtoto huyu mdogo,
ambaye Maria anamfunika vizuri na upole, ni Mungu wetu aliyejifanya siyo kitu kutokana
na upendo wake kwetu. Basi sisi tumpigie magoti kwenye pango alikozaliwa na tumwabudu
Mwumbaji wa ulimwengu aliyejifanya kiumbe, Mungu asiyeonekana ameonekana sasa katika
umbo la mwili wa mtoto, Bwana mwenyezi wa mbingu na dunia amejionyesha kuwa mdogo
na mtoto mchanga mdhaifu mwenye kuhitaji kila kitu, anahitaji hata kupendwa.
Fumbo
la kulitafakari na kuliangalia kwa jicho la imani lipo katika kukaona katoto haka
kachanga na kujiuliza: Ni kweli katoto haka ni Mungu kweli? Yaani, Mungu akaweza kweli
kuuvua ukuu wake mtukufu na wa enzi na kuonekana mbele yetu akiwa mdogo, tena mdogo
kabisa kiasi cha kuweza kubebwa mkononi na watu wote, Sababu gani? Jibu lake ndilo
ni fumbo linalodai imani ili kulielewa. Wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Eva) walidanganywa
na nyoka wa kale wakawa na shauku na hamu ya kuwa kama Mungu ili kuwa huru na kuachana
kabisa na Mungu.
Wakataka kuwa kama Mungu ili kujilinganisha na kukaa kiti
kimoja na Mungu. Wakataka kujitegemea, kuwa huru, kuwa na ukuu, uweza wa kuwa na wa
kufanya wanachokitaka wao. Dhambi hiyo ya kutaka kulingana na Mungu ilikuwa kuu sana:
yaani kule kutaka kuchukua nafasi ya Mungu na kuwa juu ya Mungu. Huko ni kumfedhi
sana Mungu. Ni zaidi ya kumtusi matusi ya nguoni. Ilitosha kabisa Mungu kutumaliza
na kutufifisha milele.
Kwa harakaharaka tu Adamu na Eva wakajikuta wamevuliwa
nguo wako uchi, maskini, na watu wa kufa. Hata hivyo, hakuna mtu yeyote ambaye angeweza
kulirekebisha kosa hili zito na kubwa sana alilokosewa Mungu la kuvuliwa nguo na kiumbe
chake. Aidha kutokana na upendo wake mkubwa kwa binadamu, Mungu hakutaka kukipoteza
milele kiumbe chake, akajifanya mwenyewe binadamu: Kwa vile kile ambacho hakikuwezekana
kwa mtu wa kawaida tu, basi kiwezekane kwa mtu ambaye si mtu tu peke yake bali ni
Mungu pia.
Ndiyo maana mtoto aliyelala uchi pale pangoni ni Mungu. Mara nyingi
tumesikia tamko hilo, lakini bado hatujagundua kikwazo, na upuuzi wa kibinadamu. Mtoto
yule mdogo anayelia, anayecheka, anayenyonya maziwa ya Mama ni Mungu! Inawezekanaje?
“Yawezekanaje kuamini kwamba mtoto huyu kuwa ni Mungu… Mungu mkuu, mwenye mamlaka,
Mungu wa milele, na kuweza kuishi kama wengine wengi wasiojua hilo, wasiotambua hilo,
na wasiosadiki hilo?”.
Kwa hiyo haiwezekani kusadiki kwamba inawezekana kuwa
na imani isiyokuwa na vikwazo, mapambano, na isiyotaka kufanya maamuzi. Ndiyo hii,
“Inawezekana kabisa kwamba wengi kutosadiki hata kuvutika kuamini eti katoto haka
ni Mungu.” Kwa hoja hiyohiyo, ndiyo alitundikwa msalabani. Yaani, Yesu hakusulibishwa
kwa sababu alihubiri upendo, la hasha, bali kwa sababu alithibitisha mwenyewe kuwa
ni Mungu kama Baba. Hii ndiyo ilikuwa sababu ya kuhukumiwa kifo.
Mtoto huyu
atakapokuwa mkubwa, na kuletewa mtu aliyepooza toka juu ya paa lililobomolewa kusudi
amponye akasema “Dhambi zako zimeondolewa” hapo wafarisayo wakiwa wamekwazwa wakasema
kwa haki “Anakufuru!” Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
(Lk. 5:21ff). Mtoto huyu atakapokuwa mkubwa atasema pia “Kabla ya Abrahamu mimi nilikuwepo”
(Yoh. 8:58) Atakaposhtakiwa kwa kuvunja sabato kwa sababu siku hiyo alikuwa anaponya
watu, atasema “Baba yangu anatenda kazi daima, na mimi pia” na hata kutokana na maneno
hayo, Wayahudi wakatafuta tena kumwua si kwa sababu alikuwa anavunja sabato, la, bali
kwa vile alikuwa anamwita Mungu Baba yake na kufanya mambo sawa na Mungu” (Yoh. 5:16-17).
Katika
kiini cha Liturujia la Neno la Mungu, kuna tafakari ya juu kabisa Maingilio ya Injili
ya Johani kwamba Neno lililokuwa tangu mwanzo likatwaa mwili na likajenga hema yake
kati yetu.
Fumbo mojawapo linalodai imani kulielewa ndilo hili la Neno kuwa
mwili (kitu). Kutambua kuwa Mungu aliumba vitu kwa kutamka Neno au jina la kitu hicho-
anga, mwanga, dunia nk. Kumbe maneno tutamkayo yanatakiwa yaumbe kitu. Aidha kuelewa
pia Neno la Mungu alitwaa mwili akakaa kwetu hapo tungepima zaidi maneno tuongeayo
– hasa maneno ya uwongo na ulaghai. Fumbo hili ni kubwa kwamba motto mchanga Yesu
ni Neno lililotwaa mwili, ni Mungu kweli.
Walimwua kwa vile alijitangaza kuwa
Mungu na hakuwa anatambulika hivyo kwa vile walikuwa na wazo la Mungu lililo tofauti,
yaani Mungu mkuu ambaye hakuna nafasi kwa udhaifu, unyonge, manyenyekesho na zaidi
Mungu anayekufa tena kufa msalabani! Mungu wa aina hiyo hapendezi kwa binadamu ambao
wanampenda Mungu mwenye nguvu, mtukufu, mshindi anayekuokoa tokana na msalaba, mungu
asiyekuwa msalabani, Mungu anayekulipa sala zako.
Binadamu wanamtafuta Mungu
wa nguvu hivyo, na siyo Mungu wa kubebwa mikononi kama mtoto. Ndugu zangu, Heri kwa
Noeli, Nawatakia mtoto Yesu kupokewa ndani yetu kwa mikono miwili, na maisha yetu
yakue katika imani yetu na kwa wengine.
2. Hali ya Matumaini:
Katika
mtoto huyu mchanga, ambaye Maria anamlaza kwa taratibu na polepole kwenye hori la
kulia ng’ombe chakula, tunamtambua kuwa yu Mwalimu, ameketi juu ya kiti chake cha
kwanza cha enzi, anaongea kwa nguvu yote mioyoni mwetu. Majivuno ya wazazi wetu wa
kwanza yalikuwa ya hali ya juu sana, na hapa unyenyekevu anaoonyesha Mungu hapa wa
hali ya juu sana, yaani kujivua kabisa nguo ya utukufu wa kimungu na kuwa mtupu kabisa,
na kujionesha kwetu katika hali ya mtoto mdogo na mchanga kabisa.
Kufanya
kwake hivyo, si tu anachukua mwili unaokufa ili kuujenga ubinadamu, bali anatuonesha
pia njia, namna ya kuweza kuwa Mungu kama Yeye. Maana yake, kama Yeye ni Mungu na
ni mtu kweli, hata sisi tulio binadamu tunaweza katika Yeye, na kama Yeye kuwa Mungu
yaani “upendo” (IYoh 4:8.16) kwani alimwumba mwanamke na mwanamue “kwa mfano na sura
yake” (Mwanzo 1:26) ili waweze kuwa kama Yeye, aliye upendo. Maana yake, hitaji la
kuwa kama Mungu, liliwekwa na Mungu mwenyewe ndani ya moyo wa binadamu.
Udanganyifu
wa adui shetani halikuwa la kumwelekeza mtu kwenye hitaji hilo la kuwa kama Mungu,
bali lilikuwa kuwaongoza binadamu yu Mungu tena Mungu mwenye kupenda mamlaka, mabavu,
utawala na siyo Mungu aliye upendo. alimchemsha kwelikweli binadamu kuwa atakuwa kama
Mungu lakini bila ya Mungu, maana yake bila ya upendo. Hapa ndipo ilipolala dhambi
ya asili inayoendelea kumtafuna binadamu had leo.
Baada ya kupiga magoti mbele
ya pango kwa kitoto kichanga, aliye mtoto wa Mungu, na ambaye katika mwili wake mdogo,
lakini “anabeba ndani yake utimilifu wa umungu” (Koloseo 2:9) sasa, tutulie mbele
yake bila papara, na kumsikiliza anapoongea kwa nguvu moyoni mwetu: ni “Bwana, ni
Mwalimu” (Yoh. 13:13) anayetuongelea, ni Mwalimu wa Upendo! Tumsikilize. (Rej. Lk.
9:29) anataka kutueleza nini?
Atazungumzia juu ya utupu wa pango lile, atatutuzungumzia
juu ya hori lile alimolazwa, atazungumza juu ya machozi yake ya kwanza aliyotoa na
ile tabasamu lake la kwanza, na yote hayo yatatusuta mioyoni mwetu na kutufanya tuonje
hali ya kawaida, ya ufukara, ya unyenyekevu, ambayo imeshasahaulika, hali hiyo inukie
tena katika maisha yetu. Labda itatufanya tusionje tena utamu wa ulimwengu huu na
kuupapalikia. Ulimwengu huu uliojaa kila maraharaha yanayomharibu binadamu na kumdhalilisha.
Alifika ulimwenguni ili kutuvuta tumfuate, kututeka kwa nguvu tamu ya upendo,
uzuri na ukweli inayoonekana katika ufukara na unyenyekevu wake. Baadaye atakapokuwa
mkubwa mtoto huyu atafundisha: “Njoni kwangu, ninyi nyote mnaoelemewa na mizigo mjifunze
kwangu kwani mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, kwani mzigo wangu ni mtamu na mwepesi
(Mt. 11:28-29).
Upole na unyenyekevu, vinatuonesha njia ya ukuu, ya nguvu ya
kweli, njia ya utukufu wa kweli. Kutoka pale pangoni, tunasikiliza mahubiri ya kwanza
ya Yesu: “Mnataka kuwa wakuu, yaani wakuu hasa? Mnataka kuwa na nguvu na mamlaka,
mamlaka hasa? Mnataka kutukuzwa haswa? Basi muwe wanyenyekevu, wapole, muwe wadogo
kama nilivyo nilivyowaonyesha mimi leo. Ukweli ni kwamba, mimi nilivyokuwa mkubwa,
mkubwa sana… nani mkubwa zaidi ya mimi niliye Mungu? Hakuna. Sasa mimi nimejifanya
mdogo tena mdogo kabisa, ili kukufundisha wewe njia ya kuwa mkubwa kama Mimi!
3.
Hali ya Upendo:
Tunakitambua kitoto hiki kichanga ambacho kwa furaha yote Maria
anakikabidhi kwa wachungaji na Majusi, kisha makundi ya watu wanaopenda ubinadamu
huu ulio fukara utakaojitoa wenyewe hadi kufa juu ya msalaba ili kuukomboa ubinadamu.
Pale pangoni panatugutia Upendo, tena upendo mkuu wa Mungu kwetu na kwangu. Kwa kweli
amezaliwa kwa ajili yangu, kwa ajili yangu Maria anamlaza mtoto pale horini, kwa
ajili yangu yuko pale, kwa ajili yangu ananyosha mikono yake, kwa ajili yangu ananifumbulia
fumbo la hori lile. Anayesimama pale pangoni kwa imani, budi atakuwa na wazo litakalompeleka
Kalvali na kwenye fumbo la upendo lililoisha pale msalabani na alilolitoa kwenye Ekaristi.
Mahali
alipozaliwa Yesu panaitwa Betlehemu, jina ambalo kwa kihebrania linamaanisha “nyumba
ya mkate” ndiyo nyumba yake ya kwanza, “hori la kulishia wanyama” ndivyo vinavyoimba
mioyoni mwetu kuwa Yeye ni Mkate ulioshuka toka mbinguni (Yoh. 6:51) atakayetakiwa
atolewe kwa ajili ya wokovu wetu. Hori lile alimolazwa ndiyo tabernakulo ya kwanza,
ambamo “Mwanakondoo” (Yoh. 1:29) anapotolewa sadaka mara ya kwanza kwa ajili yetu,
anajitoa kwetu ili aliwe: “Asiyekula mwili wangu na asiyekunywa damu yangu hana uzima…
Anayenila mimi, ataishi kwa ajili yangu” (Yoh. 6:53.57).
Kila Noeli Mama Bikira,
kwa njia ya kanisa, tunaalikwa kumshika mtoto mikononi kama wachungaji, kama Majusi,
kama kila mtu anayeingia mle pangoni. Yeye mtoto mchanga ananyosha mikono yake midogo
kwa wote ili ashikweshikwe na kubebwa na wote: Hilo ndilo fumbo la Noeli! Vingine
hiyo siyo Noeli endapo humshiki mtoto Yesu mkononi, kama humbembelezi, humbusu. Kutokana
na hilo, Yesu amezaliwa kwa ajili yako, kwa ajili yangu: “Tumepewa mtoto” (cf Is.
9:5), kwa kweli ni wetu, kweli ni wangu, ni wako!Tukifanya hivyo, tukimshika mtoto
mikononi mwetu basi maisha yetu yatabadilika.
Kutokana na hiyo, Yeye anataka
kubebwa mkononi! Kwa sababu baada ya kumshika yeye, tutaweza kuendelea kutumia mikono
yetu ileile iliyomshika ili kujilundikia mali, kujivua, na kufurahia ukuu? Utawezaje
kuangalia macho yake machanga ya kawaida na kuendelea bado kuzama katika uovu, wivu
na kila ubaya? Utawezaje kumbeba mtoto kifuani na kuendelea bado kujichafua moyo wako
na madhambi? Huko ni kujipinga kabisa. Kutokana na hiyo, kila noeli Bikira Mtakatifu
anatukabidhi mtoto wake tumshike mikono na kumbeba kifuani petu!
Tafakari hii
imeandaliwa na kuletwa kwako na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.