2012-12-22 10:04:28

Watoto kutoka Ujerumani kuonesha mshikamano wa upendo kwa watoto wanaoishi Tanzania katika mchakato wa maboresho ya huduma ya afya!


Chama cha Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli hadi Siku kuu ya Tokeo la Bwana, watapita nyumba hadi nyumba, wakiimba nyimbo za Noeli na kuomba mchango kwa ajili ya kusaidia maboresho ya huduma ya afya kwa watoto sehemu mbali mbali nchini Tanzania. Upendo huu wa mshikamano utawahusisha zaidi ya watoto nusu millioni wanaopenda kuwaonjesha watoto wenzao moyo wa upendo na ukarimu kwa kugawana hata kile kidogo walicho nacho, kama sehemu ya utamaduni wa Kikristo.

Katika kipindi cha miaka 50 tangu Tanzania ilipojipatia uhuru wake, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sekta ya afya, lakini bado kunahitajika maboresho katika huduma ya afya kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Chama cha Utoto Mtakatifu kwa kuangalia mahitaji ya watoto nchini Tanzania, kimeamua mwaka huu anasema Monsinyo Claus Kràmer, Mkurugenzi wa Utoto Mtakatifu Ujerumani kuelekeza misaada yake nchini Tanzania.

Tarehe Mosi, Januari 2013 watoto 20 kutoka Jimbo kuu la Colon, Ujerumani watahudhuria Ibada ya Misa Takatifu katika Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, sanjari na siku ya Kuombea Amani Duniani. Tarehe 4 Januari 2013 wawakilishi wawili wawili kutoka katika Majimbo 27 ya Kanisa Katoliki nchini Ujerumani watakutana na Waziri mkuu wa Ujerumani Angela Merkel kwa niaba ya watoto wengine wote wanaoshiriki katika kampeni ya Kipindi cha Noeli kwa Mwaka 2012.

Watoto hawa kila nyumba watakapoingia kwenye nyumba yoyote ile wataacha alama ya "C+M+B: Christus+Mansionem+Benedicat: maana yake: Kristo + Bariki + Nyumba. Kwa tafsiri sahihi ingekuwa: Kristo Bariki Nyumba Hii. Huu ni ukarimu kutoka kwa watoto nchini Ujerumani, mfano bora wa kuigwa hata na watoto wengine waliobahatika kuishi katika familia zenye uwezo kujenga utamaduni wa kuwasaidia watoto wenzao wanaoishi katika mazingira hatarishi, kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa dhati.







All the contents on this site are copyrighted ©.