2012-12-22 12:40:16

Vijana wawezeshwe kielimu ili walete mabadiliko katika maisha vijijini!


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameahidi kuchangia gharama za ununuzi wa jenereta kwa ajili ya kata ya Usevya iliyopo wilayani Mlele mkoani Katavi lakini amewataka wafanyabiashara maarufu katika kata hiyo wajiunge na kuchangia nusu ya gharama hizo. Alitoa ahadi hiyo Ijumaa, Desemba 21, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Usevya kwenye uwanja wa ofisi ya tarafa akiwa katika siku ya tisa ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Nakubali kuwa umeme ni changamoto kubwa katika kata hii natoa rai kwa wafanyabiashara wa hapa Usevya, kaeni chini mpange mtachangia kiasi gani ili tupate jenereta kubwa la kusambaza umeme kwa kaya 300. Tunahitaji sh. milioni 50 ili kupata jenereta la aina hii,” alisema.

“Kule Majimoto niliwaahidi kuwachangia nusu ya gharama yaani sh. milioni 25, na nyinyi pia tafuteni hiyo nusu na mimi nitatoa shilingi milioni 25/-. Lakini, hizo za kwao zitolewe kama mkopo na hizi za mbunge ziwe msaada. Tukubaliane kuwa mtarudishiwa umeme ukianza kupatikana ili jenereta liwe mali ya kijiji,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa uliohudhuria mkutano huo.

“Natoa ushauri huu kwa sababu najua tukiwaachia wafanyabiashara wamiliki hili jenereta na kuuza umeme wataweka bei kubwa na hii itawafanya watu wengine wakose huduma hii muhimu,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ambaye ni Mbunge wa jimbo la Katavi ameahidi kuwasomesha chuo cha VETA vijana 16 kutoka katika kata hiyo ili waweze kuendeleza miradi ya kikundi chao cha ujasiriamali.

“Nimependa ubunifu wa kikundi cha wajasiriamalai Usevya. Nitamwomba diwani asimamie zoezi hili, tupate vijana 16 waende VETA wakasomee upishi. Mimi nitawalipia ada na kuwanunulia vifaa vya kisasa ili waje huku kufanya catering services za nguvu,” alisema.

“Wamesema wakivuna watanunua mizinga ya kisasa. Mimi nitawapatia mizinga kulingana idadi watakayonunua. Wakinunua 10 nitawapa 10; wakinunua 20 nitawapa 20; mkinunua 100 nitawapa 100. Nataka kupitia vijana, watu wengine waone mabadiliko na waone kuwa jambo la ufugaji nyuki linawezekana,” alisisitiza.









All the contents on this site are copyrighted ©.