Ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali unapania kuboresha huduma ya afya Mkoani Mbeya
Mheshimiwa Padre Renatus Mwakanyamale, Katibu wa Afya, Jimbo Katoliki Mbeya ameishukuru
Wizara ya Afya kwa kuwa na ushirikiano mzuri na Kanisa kupitia huduma ya afya inayotolewa
na Kanisa. Licha ya kuwa na uhaba wa watumishi na vifaa lakini bado juhudi za Serikali
katika kuhakikisha tatizo hilo linapunguwa ama kumalizika zinaendelea na hivyo kutia
moyo wa kuendelea kutoa huduma hiyo.
Padre Mwakanyamale ambaye pia ni Paroko
wa Parokia ya Mbalizi amesema, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ushirikiano
na mahusiano mazuri baina ya Halmashauri za Wilaya ya Rungwe, Chunya na Mbozi ambako
Jimbo Katoliki la Mbeya linatoa huduma zake za afya kwa kuwapelekea watumishi na vifaa
tiba hali inayodhihirisha kutekeleza kwa vitendo mkataba wa makubaliano ya utoaji
wa huduma za afya kwa jamii (Service Agreement).
Aidha Padre Mwakanyamale alisema
tatizo ambalo limebakia ni ucheleweshwaji wa fedha ya ruzuku kwenda katika maeneo
ambako huduma hizo zinatolewa na hivyo kuleta usumbufu mkubwa lakini ana imani Serikali
ni sikivu italifanyia kazi kwa kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Padre Mwakanyamale
anabainisha kwamba, Jimbo Katoliki la Mbeya lina Hospitali mbili teule za Wilaya ambazo
ni Igogwe iliyopo Wilayani Rungwe na Mwambani iliyopo Wilayani Chunya, vituo vya afya
viwili ambavyo ni Mkulwe na Kisa pamoja na Zahanati 22 zikiwemo za Iyunga kwa Mbeya
mjini na Lupa, Totowe na Mbuyuni, Wilayani Chunya ambazo zipo katika mchakato wa kupandishwa
hadhi ili kuwa ni Vituo vya afya.