2012-12-22 09:03:04

Tahariri ya Padre Lombardi: Familia na Ukweli!


Hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa wasaidizi wake wa karibu mwishoni mwa mwaka, ni kati ya tafakari binafsi zinazoandaliwa kwa umakini mkubwa pamoja na kuzama katika mada ambazo amezipatia kipaumbele cha kwanza, ili kuweza kushirikisha mawazo kwa ujasiri mkubwa akitambua dhamana na wajibu wake kwa Kanisa na kwa Familia ya binadamu katika ujumla wake.

Ni mawazo ambayo kwa kawaida yanakubalika, lakini wakati mwingine yanapambana na upinzani mkubwa. Mwaka huu ameamua kuzungumzia ukweli kuhusu Familia na Uwili unaoundwa kati ya Bwana na Bibi; Majadiliano na Utangazaji wa Imani.

Padre Federico Lombardi katika tahariri yake anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu amechagua mada hizi, bila ya kugusia kuhusu miswada ya sheria, ndoa za watu wa jinsia moja au maneno yaliyoonesha ukaribu wake wa pekee kwa Familia ambazo zinakumbana na hali ngumu ya maisha wakati wa kesha la Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa iliyofanyika Milano, Kaskazini mwa Italia.

Baba Mtakatifu anauliza swali la msingi "mtu ni nani? Tofauti za kijinsia kati ya mwanaume na mwanamke ni muhimu sana kwa utambulisho wa mwanadamu na uhusiano unaojengeka kati ya: baba, mama na watoto ndani ya familia mintarafu mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Kukataa uwepo wa tofauti hizi ni kukana ukweli na kutaka kuhalalisha kwamba, mwanadamu anaweza kuchagua utambulisho wake mwenyewe, hali ambayo inapelekea kwenye mahangamizi ya utu wa mtu! Mama Kanisa anaposimama kidete kutetea tunu msingi za maisha ya kifamilia anamtetea mtu mwenyewe mintarafu ufahamu na mapokeo mbali mbali ya kidini.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anapopembua kuhusu majadiliano, Mkristo anaingia katika Jukwaa hili kama mdau mkuu wa mang'amuzi ya maisha ya binadamu mintarafu mwanga wa imani; akijitahidi kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha adili na kiutu licha ya kinzani zinazojitokeza.

Kanisa linajitosa uwanjani likiwa na imani kwamba, tafiti za ukweli kamwe hazitahatarisha utambulisho wake, kwani si kwamba mwanadamu anamiliki ukweli, bali anaongozwa taratibu ili kuweza kuufikia. Hii ni dhamana pevu na nyeti na ni sehemu ya matashi mema ya kipindi cha Noeli, kuweza kuzama zaidi ili kuangalia hali halisi ilivyo wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.