2012-12-22 07:46:01

Mwaka 2012: zawadi kuu: Sinodi ya Uinjilishaji Mpya; Mtakatifu Kateri Tekakkwitha na Maadhimisho wa Mwaka wa Imani


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika Ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli linasema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walipofika mjini Bethlehemu walimletea Mtoto Yesu zawadi tatu yaani: dhahabu, uvumba na manemane. Hizi ndizo zawadi ambazo, Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, limebahatika kupata nchini Canada. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo, Kutangazwa kwa Mwenyeheri Kateri Tekakwitha kuwa Mtakatifu sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya inawakumbusha waamini kwamba, kuamini katika Habari Njema ya Wokovu ni kukubali kupokea na kufurahia utu wa kuwa ni watoto wa Mungu kwa njia ya Kristo. Kuinjilisha ni kumtangaza Kristo anayemkirimia mwanadamu ukombozi kwa njia ya maneno na ushuhuda wa maisha. Ni mwaliko na changamoto ya kujiweka wazi katika njia ya amani na msamaha; upendo na haki; kwani Yesu Kristo amekuja kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu; kumbe Uinjilishaji Mpya hauna budi kufurahia na kushirikisha uzuri wa imani na utajiri wa dunia hii.

Mtakatifu Kateri analijalia Kanisa nchini Canada fursa ya kuwafahamu Wahindi Wekundu ambao pia ni sehemu ya Wananchi wa Canada. Ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa uwepo wao na kuomba neema ya upatanisho ili kuponya madonda ya mioyo kwa njia ya neema na rehema kutoka kwa Mungu ambaye amependa kujipatanisha na Mwanadamu, changamoto ya kuendelea kuponya yote yanayo sababisha utengano kati ya mwanadamu na kati yake na kazi ya Uumbaji.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika waamini kugundua ndani mwao ile furaha ya kuamini na kushirikisha wengine matumaini yanayobubujika kutoka katika Imani. Mungu ndiye anayeweza kuzima kiu na njaa ya mwanadamu kwa kumpatia maana ya maisha mintarafu Imani, inayomwezesha mwamini kufungua hazina ya moyo wake ili neema na baraka za Mungu ziweze kuingia na kumkomboa na vikwazo vya maisha. Ni mwaliko wa kutolea ushuhuda wa maisha mapya katika Kristo kwa kuwa wamekuwa ni watu wapya kwa neema yake, mwaliko wa kuwashirikisha wengine.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linahitimisha salam na matashi mema kwa Siku kuu ya Noeli kwa kuwataka waamini kushukuru na kushirikishana zawadi hizi kuu tatu kama dhahabu ya Uinjilishaji Mpya; manukato safi ya Upatanisho na Imani kama moshi wa uvumba unaopaa angani. Sala na tumaini kwa Mwenyezi Mungu iwakrimie waja wake upendo na huduma kwa jirani.








All the contents on this site are copyrighted ©.