2012-12-22 08:07:27

Liturujia ya Neno la Mungu kwa Siku kuu ya Noeli 2012


Mpendwa mwanatafakari wa Liturujia ya Neno la Mungu, unayeitegea sikio Radio Vatican, kwanza ninakutakieni heri na baraka tele za kuzaliwa Mwana wa Mungu. RealAudioMP3

Leo ni Krismas, ni Noeli, ni neema ya Mungu iliyofunuliwa kwetu. Kwa hakika ile ahadi ya Mungu aliyoitoa tangu zamani sasa imefunuliwa na hivi tunafurahi na kushangilia tukiimba utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Mtoto Emanueli aliye na uweza wa kifalme mabegani mwake, Mungu pamoja nasi amezaliwa kwa ajili yetu. Kanisa duniani kote linaimba “Pangoni Batlehemu amezaliwa mtoto Yesu, twendeni sote tukamwone na kumpa zawadi”

Nabii Isaya anayeishi karne ya nane Kabla ya Kristo, anaonesha katika masomo ya sherehe za Noeli jinsi Waisraeli wanavyofurahi kurudi nyumbani toka utumwani Babeli. Wanafurahi kwa sababu wamekaa chini ya kandamizo la utumwa kwa muda mrefu, na kandamizo hilo lilikuja kwa sababu wao wenyewe walishindwa kutii mausia ya Mungu wakaingia katika ugomvi kati yao na hivi wakapelekwa utumwani. Sasa Nabii Isaya akiona mwisho wa utumwa huo katika maono anaimba akisema “watu wote waliokwenda katika giza wameiona nuru kuu na wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti nuru imewaangaza”

Uaguzi huu wa Nabii Isaya unakamilika kwa kuzaliwa Masiha, Mwana wa Mungu, aliye mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele na mfalme wa amani. Enzi yake haina mwisho, atahukumu kwa haki. Na kwa hakika hakuna mfalme mwingine kabla na baada yake aliyeweza kuwa na sifa hizi.

Katika nyakati zetu nasi tuko utumwani, tuko katika taabu mbalimbali kama vile ukosefu wa mahali pazuri pa kuishi, shida ya umeme, maji, sukari, rushwa na ugomvi kati yetu, pamoja na ajali barabarani. Je haya amesababisha nani? Ni sisi wenyewe. Sasa leo Nuru imetushukia kutoka mbinguni kama tulivyokuwa tukiimba wakati wa majilio “ushukie Masiha kuwakoa watumwao”

Je, kuzaliwa kwa Bwana au kushuka kwa Nuru hii kwatufanya kweli tuonje lile pendo la kweli walilolionja Waisraeli toka utumwani Babeli? Ewe mpendwa, Mwana wa Mungu ni Emanueli anakuja kutuondolea utumwa cha msingi tuaanze pamoja naye kuacha ubaya na kutenda wema.

Kuacha ubaya na kutenda wema ni ujumbe kamambe ambao Mtume Paulo anamtumia Mtakatifu Tito akimsistizia kuwa Neema ya Mungu Mwokozi inayookoa wanadamu wote imefunuliwa kwetu na hvi kazi yetu kama twataka kuifaidi neema hiyo ni kuambatana na maisha ya uongofu, maisha ya kupokea na kuzitumia neema za Mungu pamoja nasi yaani Emanueli. Kuzaliwa kwa Kristu ni amani na uhuru kwa wana wa Mungu. Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu ni ufunuo mkamilifu wa Mungu kwetu kwa maana tangu zamani Mungu alisema nasi kwa njia ya mababu, manabii na sasa anasema nasi kwa njia ya Masiha, Mwanae mpenzi tunaye paswa kumfuata.

Mpendwa mwana Noeli, Mwinjili Luka akitupatia Habari ya Furaha, kwanza anamweka Bwana katika mazingira ya mwanadamu. Anaweka mbele yetu kwanza jambo la kijiografia na la kihistoria, akisimulia juu ya Masiha anayezaliwa wakati wa mfalme wa Kirumi Kaisari Augusto, pia anazaliwa Betlehem kijiji cha wachungaji kama ilivyokuwa imeaguliwa kwamba atazaliwa katika ukoo wa Daudi. Hili laonesha kuwa, Masiha anaingia katika maisha ya mwandamu. Pamoja na hilo pale pangoni Betlehemu anashuhudiwa na wachungaji kielelezo cha upendo wa Mungu kwa wote na hasa walio fukara na maskini, na kwa jinsi hiyo Mungu atufundisha kushinda uovu si kwa vita bali kwa upendo na msamaha.

Wote twatambua kuwa wachungaji wakati ule walikuwa ni watu wa kulala machungani, waliodharauliwa na hata hawakuruhusiwa kuingia kwenye masinagogi, walikuwa wakisadikika kuwa waongo na wagomvi. Mwana wa Mungu anaona hao ndio wapewe habari ya kuzaliwa kwake wakiwa wa kwanza. Maana yake Mungu ni kwa ajili yao na anachagua kukaa katikati yao yaani walio maskini. Mwinjili Yohane anaweka mbele ya mataifa Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na akakaa kwetu. Masiha ni Neno wa Mungu ambaye anatumwa na Mungu kwetu kwa sababu ya upendo upeo. Ni nuru ileile ambayo Nabii Isaya anaitanganza katika Agano la Kale ya kwamba, miisho yote ya dunia imeiona nuru na wokovu wa Mungu.

Mungu amefanyika mwili nasi tukauona wokovu wake na hivi tunaalikwa kusikiliza na kutenda kadiri ya mapenzi yake. Mwinjili Yohane anatupatia fumbo la umwilisho kielelezo wazi cha upendo wa Mungu, Mungu anayejishusha na kutwaa mwili wako dhaifu! Anataka kugeuza mwili wako uwe mwili wa utukufu. Kwa fumbo hili la Bwana kukaa kwetu ni fundisho la amani kwa mataifa, kumbe, kugombana ni tishio dhidi ya upendo katika jamii uliowekwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Yafaa kufikiri kidogo juu ya vita vinavyoendelea duniani. Kumbe, Neno akafanyika mwili ni nuru na amani kwa watu wote. Ni sura na utukufu wa Mungu Baba na kielelezo cha mapendo yasiyopimika kwa Mwanadamu.

Ninakukumbusha kuwa Bwana amekuja na kukaa kwetu, maana yake anakaa kwenye familia kumbe ni sherehe ya familia ni siku za kukaa pamoja Baba mama na watoto. Na kama vile ambavyo mtoto anapozaliwa tunapeleka habari ya furaha kwa majirani basi kukaa kwetu pamoja na Bwana katika familia kuwe ni chimbuko la habari njema ya furaha kama Wachungaji walivyopeleka habari njema ya furaha kwa watu wote.

Kumbuka kule Betlehemu Bwana alikosa nafasi katika nyumba ya wageni na hivi asije akakosa nafasi katika moyo wako katika sherehe hizi za Noel na daima. Nafasi ya Bwana yapaswa kutayarishwa daima kwa maisha ya sala na sakramenti. Kuna desturi ya kubatiza watoto katika sikukuu ya Noeli, yafaa kuelewa kuwa ni nafasi muhimu na ya pekee inayotayarisha mahali Bwana atakapokaa katika mtoto huyo, kumbe wazazi itunzeni nafasi iletwayo kwetu kwa njia ya ubatizo.

Ninakutakieni heri na baraka tele za Mungu leo na daima.

Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria Mama wa Mungu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.