Wafugaji na wakulima heshimianeni ili kulinda na kukuza amani, upendo na mshikamano
katika Jamii
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameahidi kuchangia sh. milioni 20 za kuanzia
ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Mwamapuli ili kiweze kusaidia kata za jirani
za Mbede na Majimoto.
Alitoa ahadi hiyo Alhamisi, Desemba 20, 2012 wakati akizungumza
na wakazi wa kata ya Mwamapuli kwenye mradi wa mashine ya kukoboa mpunga akiwa katika
siku ya nane ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
“Hapa
Mwamapuli hatuhitaji tena kuzungumzia habari ya zahanati sababu mmezungukwa na vijiji
vingi na kata nyingi. Mnahitaji kituo cha afya ili kata za jirani za Mbede na Majimoto
ziweze kunufaika,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi
aliwaambia wakazi hao kwamba wakimaliza kazi ya kuvuna, waweke mpango mahsusi wa kuchangia
matofali kwa kila kaya, na kila kijiji ili kusaidia ujenzi wa kituo hicho.
Aliwasihi
watendaji na wenyeviti wa vijiji wasiwabugudhi wananchi kuhusu michango hiyo hadi
watakapomaliza msimu wa kilimo. “Tuwaache wamalize kuvuna ndipo wachangie, tunataka
kituo hiki kiwe kimefunguliwa ifikapo mwaka 2015,” alisema huku akishangiliwa.
Pia
aliwataka wafugaji na wakulima wakae kwa kuheshimiana. “Wafugaji lazima tuendelee
kuheshimu wakulima, tusipeleke mifugo kwenye mashamba yao. Kuheshimiana ndiyo kutatuondolea
balaa la kupigana,” alisisitiza.
Wakati huo huo Waziri mkuu ameahidi kutoa
sh. milioni tano kwa wafuga nyuki 10 wa kijiji cha Mbede katika kata ya Mbede ili
ziwasadie kutengeneza mizinga ya kisasa.
Alitoa ahadi hiyo Alhamisi, Desemba
20, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mbede kwenye uwanja wa shule ya msingi
Mbede akiwa katika siku ya nane ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele,
mkoani Katavi.
Waziri Mkuu aliuliza kwenye mkutano huo wa hadhara wangapi wana
mizinga ya nyuki wakajitokeza watu hao 10. Alipowahoji kila mmoja, alibaini kuwa jumla
yao wote wana mizinga 115 na zaidi ya mizinga 60 ina nyuki lakini akabaini kuwa wote
wanatumia mizinga ya asili ya kutundika juu ya miti.
“Nataka muanze kufuga
kisasa… Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpanda itabidi usimamie zoezi la kutengeneza
mizinga hii ili kikundi hiki kiwe kichocheo cha mabadiliko kwa wengine katika kata
hii,” alisema.
“Achaneni na hiyo mizinga ya asili kwa sababu uzalishaji wake
ni mdogo, na kazi ya kuparamia ina adha zake… kwenye mizinga ya kisasa unaweza kucheki
nyuki kama wameingia kwenye mzinga kadri unavyotaka,” alisema.
Waziri Mkuu
ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi aliwaambia wakazi hao kwamba nyuki wanaweza kufugwa
kama ilivyo kwa mifugo mingine. “Wanataka kuwekewa maji, mabanda yao yanataka kusafishwa
kila mara, na hii itakuwa rahisi kama tu mtatumia mizinga ya kisasa,” alisisitiza.
Waziri
mkuu amewataka wakulima wa kata ya Mwamapuli wakubaliane kula njama na wakatae kuuza
mpunga kutoka bonde la Rukwa ili wanunuzi wote wanunue mchele badala ya mpunga.
Alitoa
rai hiyo Alhamisi, Desemba 20, 2012 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwamapuli
kwenye mradi wa mashine ya kukoboa mpunga akiwa katika siku ya nane ya ziara yake
jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Alisema kuuza mchele kutaongeza
thamani ya zao hilo na hivyo kufanya bei iwe juu. “Itabidi diwani na viongozi wengine
wakae na wananchi na kupanga bei ya kuuza mchele wao ili kuwa na sauti ya pamoja,”
alisema.
Alisema mashine hiyo ya kukoboa ina uwezo wa kukoboa magunia 400 kwa
siku kwa hiyo wana uhakika wa kusindika kile wanachokizalisha.
Waziri Mkuu
ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi aliwaambia wakazi hao kwamba wafuate kanuni bora
za kilimo na kuwasisitiza kulima mpunga kwa kufuata mistari ili kuongeza uzalishaji
wa zao hilo kwa kila ekari.