2012-12-21 07:55:51

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kipindi tafakari masomo ya Dominika, tunaendelea na safari yetu tukiwa sasa Dominika ya 4 ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa.

Mpendwa katika Dominika hii tunaongozwa na Nabii Mika, mwandishi wa barua kwa Waebrania na kama kawaida mwinjili Luka. Nabii Mika anatangaza wokovu kwa watu waliowaaminifu kwa Mungu. Anaishi karne ya nane ambapo kuna unyonyaji dhidi ya maskini unaofanywa na matajiri. Akiwa upande wa maskini anasema hawa wanyonyaji wataadhibiwa na Mungu, kumbe anatangaza tumaini kwa waliomaskini.

Nabii Mika anatangaza kuzaliwa kwa Masiha katika mji wa Betlehemu - Efrata, mji ambao ni mdogo bila thamani mbele ya watu lakini wenye thamani mbele ya Mungu, maana atazaliwa huko mfalme wa amani na mtawala wa Israeli mpaka miisho ya dunia. Efrata ni famila ndogo ya kabila la Yuda ambapo kwanza anazaliwa Daudi na Kisha Mfalme Mkuu yaani Yesu Kristo Masiha. Huyu atakuwa Mchungaji wa kondoo na mchungaji mwema. (Yn. 10) Mfalme huyu ni Mfalme wa amani kwa sababu ni mwenye upendo kwa Mungu na kwa jirani.

Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, mwandishi wa barua kwa Waebrania anawaandikia watu walioongekea ukristu na kwa namna hiyo anataka kuwaimarisha katika imani yao. Anawaambia kuwa Kristo ni yule aliyetabiliwa katika Agano la kale, kwa namna hiyo basi anakamilisha uaguzi huo anaposhuka kwetu. Anakazia mafundisho yake akiwaambia Kristo anatolea sadaka moja tu ya Kalvari kwa milele na inatosha kwa ondoleo la dhambi zetu zote. Kristo anamtii Mungu na hivi anachukua nafasi ya dini ya zamani na yeye anakuwa mlango wa utakatifu na Imani yetu ya Kikristo.

Kwa utii anakuwa kipatanisho chetu kati yetu na Mungu Baba na kwa namna hiyo anaondoa matambiko na sadaka za kale na tunaanza maisha mapya. Tukifuatilia vema mtililiko wa tafakari ya mwandishi tunaona pia sisi wenyewe baada ya ubatizo hatuko katika maisha ya zamani bali maisha mapya, maisha si kivuli ba halisia katika Masiha. Kwa njia hiyo, tunajiunga na utakatifu wa Yesu Kristo na hivi kama yeye alivyoyafanya mapenzi ya Baba yake nasi twaweza kutimiza mapenzi ya Mungu. Baada ya kazi hiyo takatifu basi matunda ni uzima wa milele na ni matokeo ya sadaka moja ya Bwana.

Katika somo la Injili tunapata kuingizwa katika furaha ya Krismasi, tunaalikwa kuweka nguvu zetu pamoja katika Kristu kwa kielelezo cha wanawake wawili, Maria na Elizabeti, ambao ni wazazi wa Yesu Kristo na Yohane mbatizaji. Mwinjili anatufundisha kuwa Elizabeti anashiriki furaha ya Maria na anatamka waziwazi kuwa Maria ni mbarikiwa! Kukutana kwa mama hawa 2 ni kukutana kwa Masiha na Yohane Mbatizaji. RealAudioMP3

Mpendwa, tunapotafakari kukutana kwa Mama hawa lazima tujiulize kwa nini Maria aende kumtembelea Elizabeti? Kwa maana kwanza kati ya kijiji cha Maria na Elizabeti kuna mwendo wa kutosha na isitoshe ni milimamilima! Lazima Maria asukumwe na jambo la maana, liletalo furaha katika maisha yake. Kwa hakika anataka kushiriki furaha ya Elizabeti aliyekuwa bila mtoto kwa muda wa kutosha sasa atapata mtoto, Mungu anatenda maajabu, kwa maana hakuna aliyetegemea tena kuwa Elizabeti atapata mimba!

Mpendwa, nasi tunafuata nini kanisani, katika jumuiya? Tunaifuata furaha ya Bwana, tunavutwa na upendo wa Mungu asemaye, njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo! Tendo la safari ya Maria si la kimwili tu bali lagusa roho, ni kwenda kwa Mungu. Kumbe, nasi tunaalikwa kwenda kukutana na wale waliotembelewa na Mungu ndio majirani zetu, wanajumuiya wenzetu na kanisa kwa ujumla. Maria anapofika kwa Elizabeti anashiriki furaha ya Elizabeti na kisha Elizabeti anashiriki furaha ya Maria na mtoto Yesu. Namna hii yapaswa kuwa maisha ya jumuiya kila mmoja lazima agawe vipaji vyake kwa wengine. Mtakatifu Ursula anasema kila mtawa awe ni hostia safi kwa mwenzake.

Mpendwa, katika Maadhimisho ya mwaka huu wa Imani ambao Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameuzindua rasmi hapo tarehe 11Oktoba 2012, tunapaswa kuwa waamini ambao si tu wa kujua yaliyomo katika Imani bali kuyaishi ili yaweze kuzaa furaha ambayo ni kwa ajili ya wengine. Imani hukolea mara mwaliko wa kufungua mioyo yetu, kiti kitakatifu cha mwanadamu unapokamilika na kuwekwa katika mtiririko wa maisha yak ila siku.

Maria yu na Bwana na Elizabeti anapokea furaha ya Bwana kwa njia ya Maria, kumbe hawa wote wa wawili wanayoimani na wa,maefungua mioyo yao kupokea furaha kuu. Ni wajibu wako ndugu mpendwa kufungua moyo wako ili kuishi zawadi ya imani iliyo ya kweli.

Nikutakie sherehe njema ya Noeli, Mtoto Emanueli anayekuja kwetu azaliwe katika moyo wako uliomwongokea yeye furaha ya milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.