2012-12-21 15:32:41

Salam za Noeli na Matashi mema kutoka kwa Papa Benedikto XVI kwa wasaidizi wake wa Karibu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa, tarehe 21 Desemba 2012 aliungana na wasaidizi wake wa karibu kama Familia, kutakiana matashi mema katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012, wakiungana pamoja kama Familia kumwabudu Mtoto Yesu ambaye ni Mungu aliyejifanya mtu ili aweze kuwa karibu zaidi na mwanadamu. Anawashukuru wote waliomwezesha kutekeleza utume wake sehemu mbali mbali za dunia.

Mwaka 2012 unaoyoyoma kwa kasi umesheheni maswali mazito, changamoto na matumaini katika maisha ya Kanisa na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Amezungumzia baadhi ya matukio haya kuwa ni hija yake ya kichungaji nchini Mexico na Cuba; mahali ambako ameshuhudia waamini wakiwa wamesheheni furaha inayobubujika kutoka katika Imani; vijana waliokuwa wamepiga magoti kandoni mwa barabara wakipokea baraka kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu karibu na Sanamu ya Yesu Kristo Mfalme, yalidhihirisha kwa namna ya pekee Ufalme wa Kristo unaojikita katika: amani, haki na ukweli; licha ya hali mbaya ya kiuchumi wanayokabiliana nayo wananchi wameonesha ari ya kutaka kujisafisha kutoka katika undani wa mioyo yao wakisukumwa na nguvu ya imani pamoja na kukutana na Yesu Kristo.

Ibada ya Misa Takatifu nchini Cuba ilionesha uwepo wa Mungu ambaye kwa miaka mingi hakupewa nafasi nchini humo, kwa hakika watu wanapaswa kufanya rejea kwenye tunu msingi ambazo zimejionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya mwanadamu kwa kukutana na Mungu wa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu amegusia pia Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, Hija yake ya Kichungaji nchini Lebanon alikokwenda ili kuzindua matunda ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, Waraka unaopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa Mashariki ya Kati, katika mchakato wa ujenzi wa msingi ya umoja na amani. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni kati ya matukio muhimu sana yaliyojiri katika mwaka huu.

Umekuwa ni muda wa kutafakari kwa kina kuhusu familia: kinzani, vikwazo na umuhimu wake katika kurithisha tunu msingi za maisha yamwanadamu kiroho na kimwili; ni shule ya umoja na mshikamano wa dhati, kwa kuishi na kusumbukiana kwa pamoja; kwa hakika familia inagusa undani wa mtu. Kinzani zinazojitokeza ni ile hali ya uhusiano tenge kati ya watu; uhusiano ambao hauwajibishi na unaokwenda kinyume cha utu, heshima, uhuru na utimilifu wa binadamu. Watu wanataka kuwa na uhuru usiokuwa na mipaka bila kufungwa na kifungo cha upendo hadi mauti; watu wanataka kuukimbia ukweli na kujifunga katika ubinafsi wao.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, mtu kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya familia na wengine, hapo anaweza kupata utimilifu wa maisha, vinginevyo, watoto wanaweza kujikuta kwamba wanakabiliwa na uwepo wa wazazi ambao wana mwelekeo tofauti kabisa na mapokeo; yaani wazazi wenye jinsia moja! Hizi ni dalili za kumong'onyoka kwa tunu msingi za kifamilia na kuporomoka kwa uhuru wa binadamu na asili yake kama mwanaume na mwanamke.

Dhana ya jinsia imepewa nafasi maalum katika Jamii inayojipambanua yenyewe badala ya Jamii kuipambanua dhana hii. Ni dhana inayopinga asili ya mtu kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Jamii inajitwalia madaraka ya uumbaji wa mwanaume na mwanamke; mwanadamu anakabiliwa na hali ya kuishi katika utupu, kinyume kabisa na asili pamoja na kazi ya kuendeleza uumbaji. Ni uhuru usiokuwa na mipaka kiasi hata cha kutotambua uwepo wa Mungu. Kinzani dhidi ya familia ni mchezo hatari unaomhusisha mtu na utu wake, kwani yeyote yule anayepigania uwepo wa Mungu anampigania pia mwanadamu.

Uinjilishaji Mpya ni juhudi za Kanisa katika kukuza na kudumisha majadiliano pamoja na kuendelea kutangaza Injili ya Kristo; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanadamu; majadiliano na Serikali pamoja na majadiliano na Jamii mintarafu mwanga wa Imani unaoonesha ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu katika historia yake. Ulimwengu bila kumbu kumbu za kihistoria unapoteza utambulisho wake. Kanisa linapojadiliana na Serikali halina majibu ya mkato, bali linapania kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili; mambo yanayoweza pia kumwilishwa katika shughuli za kisiasa.

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni kati ya mambo yanayoendelea kupewa kipaumbele na Mama Kanisa katika maisha na utume wake; majadiliano yanayosimikwa katika uhalisia wa maisha na mshikamano wa dhati. Ni mahali pa kushirikishana Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Biblia pamoja na kuangalia matatizo na changamoto zinazomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Jamii, Serikali na Kanisa waweze kuwajibika kwa pamoja katika kulinda na kudumisha: ukweli, haki, amani, misingi ya maadili na utu wema. Ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kusaidiana ili kujisafisha na hatimaye, kutajirishana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao za msingi zinazojikita katika ukweli na amani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna sheria mbili zinazoratibu majadiliano ya kidini, yaani majadiliano yasilenge kumwongoa mtu bali kufahamiana; hapa Kanisa linatofautisha kati ya Uinjilishaji na utume wake. Pili ni kuimarisha ukweli uliofikiwa na pande hizi mbili katika utambulisho na makubaliano yake, ili kuweza kufikia umoja katika ukweli. Wakristo wanatambua kwamba, Kristo ndiye Ukweli wanaoutafuta na kuukumbatia kwa dhati, kiasi cha kuambatana na kusonga mbele na Kristo kwa ujasiri mkuu kwani Yeye ni mwanga wa ukweli.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Uinjilishaji Mpya ni mchakato wa kumtambulisha Kristo kama Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo ili kumfahamu zaidi ili aweze kuzima kiu na udadisi wa wafuasi wake, kwa kuwafungua macho ili kuona matendo makuu ya Mungu.

Ili Neno la Mungu liweze kuota mizizi yake kuna haja kwa mwamini kuonesha moyo wa unyenyekevu, kwa kutamani kumfahamu zaidi Kristo na hatimaye kukutana naye ndani ya Kanisa, sehemu ya Fumbo la Mwili wake Mtakatifu; tayari kujenga na kuimarisha umoja katika maisha wakiwa macho zaidi. Licha ya umaskini na mapungufu yake, Kanisa anasema Baba Mtakatifu halina budi kuonesha uhai, ili kuzima kiu na shauku ya mwanadamu inayomtafuta Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa wasaidizi wake wa karibu kwa kuwatakia kheri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.