Noeli kiwe ni kipindi cha kukuza na kuimarisha udugu, umoja, furaha, amani, matumaini,
upendo na mshikamano!
Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli linawaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kusimama
kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, hasa kwa wanyonge na watu wasiokuwa na
sauti. Inasikitisha kuona kwamba, kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, zawadi ya
uhai inaendelea kuwa mashakani, kiasi kwamba, kuna baadhi ya watu hawaoni tena thamani
ya maisha, kiasi cha kuichezea wanavyotaka!
Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho
ya Siku kuu ya Noeli, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga
na kuimarisha umoja, udugu, mshikamano wa upendo na ukarimu, kama njia muafaka ya
kumkaribisha tena Mtoto Yesu anayezaliwa katika maisha na mioyo ya watu.
Maaskofu
Katoliki Uruguay wanasema, furaha ya Mama Kanisa kwa wakati huu inabubujika kutokana
na kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia; anayekuja kumshirikisha mwanadamu furaha,
upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu.
Ni mwaliko wa kutoka katika matendo ya
giza na mauti na kuanza safari inayomwelekeza mwamini katika furaha inayothamini
na kuendeleza zawadi ya maisha, dhidi ya tamaduni za kifo zinazoendelea kuibuka kwa
nguvu ya ajabu. Watu wajifunze kuthamini maisha ya binadamu katika hatua mbali mbali
za makuzi yake; wakuze fadhila ya matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya na daima
wajitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu.
Hii ndiyo
njia bora zaidi ya kuweza kuadhimisha Siku kuu ya Noeli kwa kukataa kabisa kishawishi
cha utengano na uvunjaji wa sheria za nchi. Ni furaha inayojikita katika utambuzi
wa uwepo wa Mungu kati ya watu wake na kwa njia hii, Kanisa linaweza kuwafikia watu
mbali mbali katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili kuwaonjesha ile furaha ya
kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, Mfalme wa Amani.
Ni matumaini ya Maaskofu Katoliki
Uruguay kwamba, Siku kuu ya Noeli itawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kugundua na kukuza ndani mwao ari na moyo wa udugu, furaha, ukarimu, matumaini,
amani na maendeleo ya kweli, yanayojali utu na heshima ya kila mwanadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu.