Mwaka wa Imani uwe ni kichocheo cha kuifahamu, kuiimarisha na kuimwilisha imani katika
matendo ya huruma na upendo!
Askofu Alfred Agyenta wa Jimbo katoliki Navrongo, Ghana, katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, anawaalika Watu wa Familia ya Mungu Jimboni mwake, kutumia vyema maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, ili kuifahamu, kuiimarisha na kuimwilisha Imani yao kwa njia ya
vitendo; daima wakijitahidi kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kukumbatia fadhila za
maisha adili.
Uwe ni Mwaka
wa Neema na Baraka. Waamini washirikiane kwa karibu zaidi na viongozi wao wa maisha
ya kiroho, ili kufanikisha mikakati na malengo ya Mwaka wa Imani pamoja na kufanya
tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Msalaba ambao utatembezwa Jimboni humo wakati wote
wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Waamini watambue na kuthamini Msalaba unaonesha
upendo wa hali ya juu kabisa ulioneshwa na Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko
wake ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Mwaka
wa Imani iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu tunu msingi za maisha bora
ya Familia kwa kujitahidi kuiga Mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu,
iliyoonesha imani na matumaini makubwa kwa Mwenyezi Mungu; ikawa ni kielelezo thabiti
cha Injili ya Upendo kwa Mungu na Jirani; Ibada na bidii ya kazi. Familia ya Kikristo
ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu, haki, amani, upendo, mshikamano
na msamaha wa kweli. Kwa maelezo haya, Familia inakuwa ni Hekalu, mahali panapoonesha
na kudhihirisha uwepo wa Mungu.
Familia ya kweli na inayodumu, ni ile inayosali
kwa pamoja. Mwaka wa Imani uwe ni chachu kwa Wanafamilia kushiriki kwa pamoja katika
Maadhimisho mbali mbali ya Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi katika Maadhimisho ya
Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; bila kusahau
Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu; tayari
pia kumwilisha tunu hizi katika uhalisia wa maisha, kwani hii ni Imani katika matendo.
Waamini
wajifunze kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu kwa pamoja. Wazazi watambue
na kuthamini wajibu wa kuwafunza na kurithisha Imani pamoja na tunu msingi za kimaadili
kwa watoto wao. Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki iwasaidie wazazi kujiandaa vyema
kuwashirikisha na kuwarithisha watoto Imani wanayoungama, wanayoiadhimisha, wanayoimwilisha
na kuisali, ili iweze kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya watoto wao tangu mwanzo,
kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo!
Waamini wanakumbushwa kwamba, Parokia
ni Jumuiya ya Waamini inayoonesha uhai, maisha na utume wa Kanisa mahalia. Hapa waamini
wanapata fursa ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa; wanajenga na kuimarisha uhusiano
wao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha
utamaduni wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Wahamasike kufanya hija za
maisha ya kiroho ili kujipatia rehema kamili zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, kwa kutekeleza masharti yaliyowekwa, yaani: kupokea Sakramenti
ya Upatanisho, Ekaristi Takatifu na Kusali kwa nia ya Baba Mtakatifu. Mwaka wa Imani,
ulete hamasa ya kutolea ushuhuda makini wa Imani katika matendo.
Waamini wajifunze
kwa moyo sehemu muhimu za Ibada ya Misa Takatifu ambazo mara nyingi zinaimbwa: kwa
mfano: Utukufu, Kanuni ya Imani na Sala ya Baba Yetu ambayo kimsingi ni muhtasari
wa Mafundisho Makuu ya Yesu. Hii ni hazina ya Imani.