Mapigano kati ya wakulima na wafugaji yapelekea watu 30 kupoteza maisha nchini Kenya
Zaidi ya watu thelathini wamepoteza maisha kutokana na mapigano ya kikabila kati ya
watu kutoka kabila la Pokomo na wale wa kabila la Orma Wilayani Mto Tana, nchini Kenya.
Choko choko za makabila haya mawili ya wakulima na wafugaji zinatokana na kugombea
mahali pa kulishia mifugo dhidi ya wakulima pamoja na mahali pa kunyweshea mifugo
yao, hali ambayo wakati mwingine imesababisha uharibifu mkubwa wa mashamba ya wakulima.
Mapigano
kati ya wakulima na wafugaji kati ya Mwezi Agosti na Septemba 2012 yalipelekea watu
zaidi ya mia moja na kumi kupoteza maisha yao. Kardinali John Njue, Rais wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Kenya ameitaka Serikali kuhakikisha kwamba inachukua hatua madhubuti
ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na kutafuta chanzo kikuu kinachopelekea
mapigano ya kikabila nchini Kenya, ili tiba muafaka iweze kupatikana, watu waishi
kwa amani na utulivu.
Kuzagaa kwa silaha za moto ni kati ya mambo yanaopelekea
mauaji ya watu wengi wakati wa mapambano kati ya wakulima na wafugaji. Wachunguzi
wa masuala ya kiasiasa wanabainisha kwamba, kuna baadhi ya wanasiasa wanatumia kinzani
na migogoro ya kikabila kwa ajili ya kujijenga kisiasa!