Uinjilishaji Mpya ni utume unaovaliwa njuga na Mama Kanisa wakati huu!
Mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu uwezo wa kusikiliza kwa makini na hatimaye
kutambua ujumbe unaokusudiwa kwake. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uwasaidie waamini
kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, taa inayoangazia mapito
ya maisha yao. Mama Kanisa anatambua umuhimu wa Uinjilishaji Mpya, dhamana ambayo
inafanyiwa kazi katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Lakini kwa
bahati mbaya, Ulimwengu unaonekana kana kwamba, umepoteza ile hamu na uwezo wake wa
kusikiliza. Mwanadamu hapendi tena kusikia habari kuhusu Mwenyezi Mungu, wanataka
hata kumwondoa katika maisha na vipaumbele vyao! Ni mtu aliyekengeuka anayependa kukumbatia
utamaduni wa kifo; Familia kwake, haina thamani tena; kazi si kipimo cha utu na ukamilifu
wa mwanadamu, bali bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni; uchumi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia ndizo mada zinazopamba masikio ya mwanadamu katika ulimwengu
wa utandawazi.
Watu hawajisikii tena kujenga na kudumisha uhusiano wa kweli
na wa dhati, kwani wanaogopa kuwajibika. Kwa hakika, ulimwengu unahitaji maneno yanayotibu
na kuponya! Mwanadamu anahitaji neno la matumaini ili kuvunja kimya kinachoendelea
kutawala katika maisha ya mwanadamu hata pengine ndani ya Kanisa lenyewe!
Hii
ni sehemu ya barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malta wakati huu
wa Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa anaposubiri kwa hamu kuzaliwa kwa Yesu Kristo
Mkombozi wa Ulimwengu. Neno linaloponya na kumrudishia mwanadamu uwezo wake wa kusikia
na kuwasiliana na wengine ni Habari Njema ya Wokovu, Injili ambayo ni Kristo mwenyewe!
Mwenyezi Mungu anaipenda dunia, ndiyo maana amemtuma Mwanaye Mpendwa yesu
Kristo, aje kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Yesu ni Neno
linaloponya! Watu wanahamu ya kukutana na Yesu Kristo anayewapatia maana ya maisha,
amani na utulivu wa ndani; anawakirimia furaha na matumaini.
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita anasema, hiki ndicho kiini cha Uinjilishaji Mpya, unaopania
kumwonesha mwamini upya wa kukutana na Yesu, licha ya pilika pilika na changamoto
za maisha katika ulimwengu wa utandawazi. Huu ndio utume unaopaswa kutekelezwa na
Mama Kanisa, Ole wake, kama Kanisa litashindwa kufanya hivi.
Jambo la msingi
ni kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linapenya hadi kugusa moyo wa mwanadamu, dhamana
inatìyohitaji kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mikakati na shughuli za kichungaji.
Waamini wachangamkie usomaji, tafakari na umwilishaji wa Neno la Mungu katika
uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Ni mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kina,
kwani kwa njia hii, watu wanaweza kuguswa na uwepo wa Mungu katika hija ya maisha
yao! Imani katika Yesu inaponya, kama inavyojionesha katika matukio mbali mbali kwenye
Maandiko Matakatifu; lakini jambo la msingi ni kuanzisha mchakato wa majadiliano na
Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala!
Kanisa halina budi kujibu kilio cha watu wanaoendelea
kuelemewa na uzito wa Misalaba yao ya maisha. Ni watu ambao wamejeruhiwa: kimaadili,
kiutu na kiimani. Kama yule Msamaria mwema, Kanisa halina budi kuwapatia tiba ya kweli
kwa njia ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Kanisa liendelee kufanya hija
na wote wanaoteseka na kudhulumiwa, waliojeruhiwa, ili aweze kuwagusa na kuwaponya
katika shida na mahangaiko yao.
Katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya, Mama
Kanisa anapenda kupangusa machozi ya wale wanaolia na pale inapowezekana kuzuia kabisa
machozi haya yasimwagike! Uinjilishaji Mpya hauna budi kujikita katika maisha ya mwanadamu
kwa kuanzia kwenye: familia, maeneo ya kazi, urafiki, umaskini pamoja na majaribu
mbali mbali ya maisha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linasema kwamba, hakuna
Uinjilishaji Mpya pasi na toba na wongofu wa ndani, ili kuchuchumilia utakatifu wa
maisha. Dhamana hii inawezekana pale tu, waamini watakapoonesha moyo wa toba, ili
kufungua masikio ya mioyo yao, kusikiliza kwa umakini Neno la Mungu na kupokea nguvu
ya Kristo inayoponya!
Kipindi cha Majilio na hatimaye, Noeli ni Maandalizi
ya Ujio wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kukaa
tumboni mwa Bikira Maria, nyota ya Uinjilishaji Mpya. Alisaidie Kanisa kutekeleza
wajibu pamoja na kukabiliana na changamoto mbali mbali katika azma ya Uinjilishaji
Mpya, ili viziwi waweze kusikia Habari Njema ya Wokovu na Bubu waweze kutangaza utukufu
na matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!