2012-12-20 11:14:09

Papa ajibu Ombi la Gazeti la TIMES: asema Wakristo na Watu wenye mapenzi mema wajitahidi kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya mshikamano wa upendo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amekubali na kujibu ombi la Gazeti la TIMES kuwamegea wasomaji wa Gazeti hili mawazo yake mintarafu kitabu chake kuhusu Simulizi za Utoto wa Yesu, kilichochapishwa hivi karibuni, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu amekwisha wahi kupokea maombi kama haya kutoka kwa Shirika la Utangazaji Uingereza, yaani BBC baada ya kuwa amehitimisha hija ya kichungaji nchini Uingereza. Ombi kama hili pia lilikwisha kutolewa na Kituo cha Televisheni cha Taifa, Italia, alipokuwa anajibu maswali katika Maadhimisho ya Ijumaa kuu.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kushirikisha mawazo yake wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, kwa kuhakikisha kwamba, waamini wanajihusisha na maisha duniani kwa kumpatia Mungu kile kilicho cha Mungu na Kaisari, yale yaliyo ya Kaisari bila kumwingiza Yesu katika majaribu kama walivyotaka kufanya Mafarisayo. Waamini wasichanganye mambo ya kidini na kidunia kwa nia ya kuchuma mali na kujipatia utajiri. Yesu alitumia fursa ile kuweka bayana kuhusu utawala wake kwamba, haukuwa ni wa dunia hii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Simulizi za Maisha ya Utoto wa Yesu katika Agano Jipya zinaonesha kwamba, alizaliwa wakati wazazi wake wakishiriki katika zoezi la kuhesabu watu, wakati wa utawala wa Kaisari Augusto. Mtoto Yesu alizaliwa kwenye mazingira duni kabisa, lakini, huyu ndiye anayeleta amani duniani inayopita nyakati na mahali. Ni Mfalme anayeshinda dhambi na mauti kwa njia ya mateso na kifo chake.

Kuzaliwa kwa Yesu ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kuthamini zawadi ya maisha; ni fursa ya kuchunguza dhamiri hasa zaidi kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, ambao umesababisha madhara makubwa katika maisha ya watu na kile ambacho watu wanaweza kujifunza kutokana na unyenyekevu, umaskini na ukawaida wake. Noeli kiwe ni kipindi cha kusoma na kufanya tafakari ya kina kuhusu Maandiko Matakatifu, ili kumtambua Kristo ambaye ni Mungu kweli na Mtu kweli.

Wakristo popote pale walipo, wajitahidi kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi: kwa kupambana na umaskini na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mwanadamu; watumie vyema rasilimali ya dunia na wawe ni watunzaji bora wa mazingira, wakionesha mshikamano wa upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kujipatia utimilifu wa maisha.

Kila mtu anachangamotishwa kuwa ni mjenzi wa msingi wa haki na amani. Wakristo washirikiane na waamini wa madhehebu na dini mbali mbali katika kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa Mungu na katika dunia hii. Wajitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na kamwe wasiabudu miungu wa uongo.

Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni kielelezo cha mwanzo mpya dhidi ya utawala wa Mfalme Kaisari Augusto ambao hakuwa na mpinzani kwa karne nyingi. Yesu ni Mfalme wa Amani na Matumaini kwa wote wanaoishi katika wasi wasi na hali ngumu ya maisha. Kutoka katika Pango alimolazwa, anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kushikamana ili kujenga dunia iwe ni mahali pazuri pa kuishi.







All the contents on this site are copyrighted ©.