Muasisi mkuu wa maisha, furaha, upendo, amani ni Mungu ambaye amejifanya mtoto katika
Nafsi ya Yesu Kristo!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi tarehe 20 Desemba, 2012 amewashukuru
wajumbe wa Chama cha Vijana Wakatoliki Italia waliofika kumtakia matashi mema kwa
Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2012. Kauli mbiu ya majiundo endelevu ya vijana hawa inawaalika
kwa kusaidiana na walezi wao kumtafuta "muasisi", ili hatimaye, waweze pia kusaidiana
na vijana wengine.
Baba Mtakatifu anafahamu kwamba, vijana hao wanamtafuta
muasisi wa maisha atakayewasaidia kuishi vyema, wakiwa wameridhika wao pamoja na wenzi
wao! Huyu ni Mwenyezi Mungu ambaye amewafunulia uso wake; amewaumba kwa sura na mfano
wake, lakini zaidi, amewakirimia Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo, aliyejinyenyekesha
na kuwa kama mtoto atakayezaliwa tena katika kipindi cha siku chache kuanzia sasa.
Ni mtoto aliyekuwa na kukomaa kama vijana hao, akafanya hija ya maisha hapa duniani
ili kutangaza upendo wa Mungu unaowawezesha watu kuwa wema na wenye furaha na wakarimu.
Mungu
ndiye muasisi wa chemchemi ya furaha ambayo haipatikani kwenye michezo, kati ya marafiki
na wazazi wanaowapenda fika na kuwamegea furaha, lakini Yesu ndiye Rafiki yao mkubwa
anayejaza mioyo yao kwa furaha ya kweli na endelevu katika maisha yao yote; changamoto
kwa vijana kujitaabisha kumjifunza, kumfahamu na kujadiliana naye ili kuweza kuridhika
katika maisha na kwa njia hii, wataweza pia kushinda machungu madogo madogo ambayo
wakati mwingine yanakuwemo ndani ya mioyo.
Vijana kama wanamtafuta muasisi
wa maisha, kamwe hawawezi kujifungia katika ubinafsi wao, bali wanapaswa kujibidisha
kutafuta mema na kujisikia kwamba, kuna mtu anayewatakia mema katika hija ya maisha
yao, jambo msingi linalomwezesha mwanadamu kuishi vyema; lakini pia vijana hawa wanapaswa
kufahamu namna ya kupenda wengine, kuthamini zawadi ya maisha kwa wote lakini zaidi
kwa wale wanaokumbana na hali ngumu ya maisha. Yesu kwa njia ya mfano wa maisha yake,
amewawezesha waamini kufahamu upendo wa Mungu ambao hauna mipaka na kwamba, anataka
kila mtu aweze kuishi kwa furaha.
Baba Mtakatifu anawashukuru Vijana Wakatoliki
Italia kwa kuchangia gharama za kuendesha mradi unaopania kuwasaidia watoto wanaoishi
katika mazingira magumu, nchini Misri. Kwa hakika, vijana hawa wanatafuta chemchemi
ya amani katika maisha yao, ambayo kamwe haiwezi kupatikana kwa juhudi za mtu mmoja,
lakini wafahamu kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayeweza kuwapatia amani ya kweli na
yenye kudumu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha shukrani
zake kwa vijana hawa kwa kuwataka kutoa nafasi katika maisha yao kwa ajili ya uwepo
wa Mwenyezi Mungu ambaye atawasaidia kubomoa kuta za ubinafsi zinazochafua uhusiano
kati ya watu na kati ya mataifa na hatimaye, kuibua ndani mwao hamu ya kutaka kujipatanisha,
kusameheana na kudumisha amani hata kwa wale ambao wana moyo mgumu kama wa jiwe!
Baba
Mtakatifu anawataka vijana kumtafuta muasisi wa tunu hizi msingi kwa kushirikiana
na wenzi wao shuleni na katika michezo. Wasaidiane kumtafuta Muasisi mkuu wa maisha,
furaha, upendo, amani, kwani hatimaye watagundua kwamba, yuko kati yao na huyu ndiye
Mungu aliyejifanya mtoto katika Nafsi ya Yesu Kristo.