2012-12-20 08:41:51

Jimbo Katoliki la Mbeya Tanzania linapania kuanza ujenzi wa Chuo Cha Uuguzi, Wilayani Rungwe wakati wowote kuanzia sasa!


Kama wasemavyo wahenga kuwa machozi ya mtu mzima hayaendi bure ndivyo ilivyotokea kwa Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo katoliki Mbeya, kwa Serikali ya Mkoa wa Mbeya kuhusu ardhi ya Kijiji cha Lupata aliyoanza kuililia tangu mwaka 1992 kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kwa kujenga chuo cha uuguzi na uganga bila mafanikio hatimaye, kimesikika baada ya kukabidhiwa rasmi ardhi hiyo na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.

Askofu ametoa kilio chake kwa serikali na kuhoji sababu ya kukwama kwa mchakato huo hata alidiriki kusema endapo ardhi hiyo ya Mungu imekuwa na mlolongo mkubwa kwa maneno yaliyozoeleka Serikali kuwa ' mchakato' unaendelea basi itafika wakati Kanisa litahamishia ujenzi wa Chuo hicho cha Uuguzi katika maeneo mengine.

Askofu Chengula ametoa kilio chake katika Jubilei ya Fedha ya miaka 50 tangu kufunguliwa kwa Hospitali ya teule ya Wilaya ya Igogwe inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya Mwaka 1962 ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela alisema, wanaozuia mchakato huo kukamilika “washindwe na walegee” na ardhi itatolewa baada ya wiki moja na alimsihi Askofu Chengula atulie na alale usingizi akiwa na uhakika wa kupata eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa makabidhiano ya eneo hilo, Meela amesema baada ya kusikia mahubiri ya Askofu kutoa kilio chake kwa uchungu aliona ipo sababu ya kufanya haraka kufuatilia suala hilo na kulikamilisha na hivyo baada ya kupitia nyaraka za awali na kupata matokeo ya tume ya uchunguzi iliyoundwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Rungwe aliamua kutoa ardhi kwa niaba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye mwenye ardhi kikatiba.


Amesema kazi yake kubwa kama Mkuu wa Wilaya ni kusimamia haki na sheria na kwamba katika suala la ardhi hiyo aliangalia taratibu zinasemaje na baadaye alichukuwa maamuzi baada ya kupima manufaa ya suala lenyewe kwa umma anayoiongoza. "Nyaraka zilionesha kuna ubabaishaji mwingi kwa sababu taratibu zote za kutuma maombi zilifuatwa kuanzia ngazi ya Kijiji, nikaona Rungwe tuna upungufu wa wauguzi 128, kumbe, Chuo kitakuwa mkombozi katika Zahanati na Vituo vya Afya ambavyo vina upungufu mkubwa wa wataalamu kwa hiyo ninakukabidhi ramani hii Baba Askofu anzeni mara moja kujenga baada ya Desemba 22 watakapokuja watu wa upimaji na ahadi ya Watoto wa kijiji hiki na Rungwe kwa ujumla kupewa kipaumbele usisahau,"amesema Mkuu wa Wilaya.


Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa, anao mzigo mkubwa wa wanafunzi zaidi ya 4,000 kati ya 5,000 waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ambao wapo wanazurula mitaani baada ya kuchaguliwa wanafunzi 800 kati yao kuendelea na kidato cha tano.

Askofu Chengula ameishukuru serikali na kumtaka Mkuu wa wilaya kufikisha salam zake kwa serikali yote ya Wilaya,kwa Mkuu wa Mkoa na Rais Kikwete kwa kumkabidhi ardhi hiyo kwa ajili ya manufaa ya watanzania kwani wataalamu watakaosoma hapo watakuwa ni watoto wa watanzania.

"Watoto watakaosoma hapa ni wa kwetu na chuo kitakuwa hakifungamani na imani za kidini,itikadi za kisiasa,kabila wa rangi, na watakaokwenda kuwahudumia ni watu wa imani mbalimbali,itikadi za kisiasa tofauti na hata wale waliokuwa wakipinga kanisa kupewa ardhi watahudumiwa bila ubaguzi, watoto watapata ajira, wakazi wa hapa wataongeza vipato kwa ajili ya nyumba, biashara, usafiri na mengine mengi na tatizo la upungufu wa wauguzi na waganga litapungua," Amesema Askofu.

Aliongeza; “Leo sina la kusema mtoto tumempata tumlee wote...kilio changu kilikuwa kumpata mtoto huyu...ninawaombea hata wale waliokuwa wanakataa kutoa ardhi wakiuguwa watibiwe...ningetoa mkono wa shukurani kwenu nyote lakini natoa baraka kwenu nyote,watakaofanyakazi na watakaofika kusoma."

Akisoma risala mbele ya mkuu wa wilaya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Igogwe, Dr. Oyeti Mwakosya chuo kinatarajia kuanza na wanafunzi 90 wa ngazi ya cheti kutokana na mipango ya serikali na wanatarajia kuendelea kutoa kozi za ngazi ya stashahada na shahada kwa wauguzi na kwamba ujenzi wa chuo ni faraja kwa Wilaya na Jimbo Katoliki la Mbeya.

Chifu wa Kijiji cha Lukata alimshukuru Askofu Chengula na Mkuu wa wilaya kwa kushirikina nao hadi kuha,kikisha ardhi hiyo inapatikana kwani uwepo wa chuo hicho ni bahati kubwa kwao na kwamba watu wake wote wamepokea tukio hilo la kihistoria kwa furaha zote na ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la Askofu kukabidhiwa rasmi ardhi ambapo zaidi ya machifu 12 walishiriki.

Na Thompson Mpanji, Rungwe.









All the contents on this site are copyrighted ©.