2012-12-19 10:54:07

Vatican inaendelea kujizatiti katika misingi ya ukweli na uwazi katika matumizi ya rasilimali ya Kanisa


Rasilimali mbali mbali zinazomilikiwa na Kanisa ni kwa ajili ya kuliwezesha Kanisa kutekeleza utume wake, kwa kuzingatia kanuni ya: ukweli, uwazi na umakini katika matumizi yake. Ni maneno ya Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa kuzindua Kanuni Mpya za Usimamizi na Matumizi ya Idara ya Fedha na Uchumi mjini Vatican, hapo tarehe 18 Dsemba 2012.

Baba Mtakatifu Paulo wa Sita, katika mabadiliko makubwa aliyofanya kwenye Makao Makuu ya Vatican ni kuanzisha Ofisi ambayo ingewajibika katika kuratibu shughuli mbali mbali za kiuchumi mjini Vatican; kwa kuhakikisha kwamba, inakuwa na ufahamu wa kutosha; inadhibiti, angalia na kuratibu shughuli zote za vitega uchumi na fedha zinazoendeshwa na Vatican.

Papa Paulo wa Sita alitaka kuboresha shughuli za Kanisa ili ziweze kuendana na asili na dhamana ya Kanisa sanjari na kujitegemea, huku likiendelea kutekeleza wajibu na dhamana yake ya kuendeleza Ibada, kazi za kichungaji na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Vitega uchumi vinapaswa kuwasaidia Makleri na wadau wa utangazaji wa Injili kutekeleza wajibu wao barabara, mintarafu Sheria za Kanisa. Kanisa na Taasisi zake lina haki ya kununua, kumiliki, kuuza na kusimamia mali.

Kardinali Bertone anakumbusha kwamba, Kanisa kimsingi halina mali, bali linamiliki mali zote hizi kwa njia ya Mashirika na Taasisi zake. Ndiyo maana Taasisi ya Fedha na Uchumi ya Vatican inayo dhamana nyeti katika maisha na utume wa Kanisa. katika miaka ya hivi karibuni, Idara hii ilipoteza mwelekeo wa shughuli zake na kuwa kama Benki ya Vatican, badala ya kuwa ni mshauri mkuu katika kupanga na kuratibu shughuli za uchumi na fedha.

Ndiyo maana Kanuni na Taratibu Mpya za Fedha na Uchumi Vatican zinapania kurudisha asili ya chombo hiki kinachosimamia shughuli zote zinazofanywa na vitengo na idara mbali mbali mjini Vatican, chini ya uongozi wa Katibu mkuu wa Vatican atakeyeridhia mwenendo na programu zake. Kanuni hizi mpya zilipitishwa mwezi Februari 2012 wakati Vatican ilipoamua kwa dhati kabisa kutekeleza sheria na kanuni za kimataifa kuhusu udhibiti wa fedha, changamoto ya kuendelea kuwa wakweli na wa wazi katika shughuli za uchumi na fedha zinazoendeshwa na Vatican.

Kardinali Bertone anasema kila kitengo na mhusika anapaswa kuwajibika katika utekelezaji wa shughuli mbali mbali za kiuchumi. Kutokana na madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa, Vatican itaendelea pia kubana matumizi taratibu ili kuweka sawia mapato na matumizi. Kila mtu anawajibika kuhakikisha kwamba anasaidia kudumisha utume wa Kanisa kwa ujumla sanjari na juhudi za mchakato wa kuifanya Vatican iweze kuaminika zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.