Umaskini, ujinga, rushwa na ufisadi visiwalazimishe wananchi kukubali kukumbatia utamaduni
wa kifo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limeonya dhidi ya Kampeni ya kudhibiti ongezeko
la watu inayoendeshwa na Serikali pamoja na Mashirika ya Kimataifa nchini humo kwa
kusema kwamba, Nigeria haina tatizo la ongezeko kubwa la watu kama wanavyodhani, kinyume
chake ni kutaka kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo ambayo madhara yake ni makubwa
kwa siku za usoni.
Sera za uzazi salama ni hatari kwa ustawi na maendeleo
ya nchi kwa siku za usoni anasema Askofu Gabriel Dunia, Mwenyekiti wa Tume ya Afya,
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, alipokuwa anazungumzia kuhusu msimamo wa Kanisa
Katoliki nchini Nigeria kuhusiana na masuala ya Familia pamoja na udhibiti wa vifo
vya Wanawake Wajawazito nchini Nigeria. Umaskini, ujinga, rushwa na ufisadi visiwatumbukize
watu katika janga kwa kukubali kutekeleza sera ambazo ni kinyume kabisa cha maadili
na utu wema.
Nigeria inahitaji kuwa na viongozi wenye mipango thabiti, wanaoweza
kutumia vyema rasilimali na utajiri wa nchi katika kupambana na changamoto mbali mbali
zinazokwamisha maendeleo ya wananchi wa Nigeria. Kuna haja ya kuwa na mgawanyo sawa
wa rasilimali ya nchi kwa ajili ya mafao ya wengi. Wananchi wanapaswa kuwa makini
na sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo sanjari na utoaji mimba.
Watu waelimishwe
kuhusu mpango wa uzazi kwa njia asili, dhamana na wajibu wa wazazi katika maisha ya
ndoa na familia ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika
masuala ya kifamilia badala ya kujikita katika kuhamasisha watu kukumbatia utamaduni
wa kifo!