Mapadre mtakuwa maskini sana ikiwa kama mtaanza kujiahangaikia, kujitafuta na kutopea
katika ubinafsi!
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, tunaendelea kuambatana na Askofu mkuu Yuda Thadeus
Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania anayetupatia tafakari ya kina kuhusu unabii
na madai yake na Makasisi wanapaswa kuwa ni Askari wa Kristo, tayari kutekeleza utume
wao bila ya kujibakiza wala kumezwa na malimwengu.
Leo katika
makala haya, anaendelea kupembua maana ya kukesha katika maisha ya Familia ya Mungu,
yaani kuwa tayari daima kutekeleza mapenzi ya Mungu, kushughulikia na kuchuchumilia
maisha ya uzima wa milele. Ni mwaliko wa kutumia vyema elimu, karama na vipaji mbali
mbali ambavyo wamekirimiwa kwa ajili ya Mungu na Kanisa lake. Popote pale Padre anapotumwa
lazima ajitahidi kujenga nyumba yake ambayo ni Kanisa, kwa kulipenda, kulitokea jasho,
kulitumikia na kulihangaikia kwani ndivyo inavyotakiwa na Kristo mwenyewe.
Askofu
mkuu Ruwaichi anawakumbusha Mapadre kwamba, watakuwa maskini sana pale watakapojitafuta
na kujihangaikia wenyewe na hatimaye kutopea katika ubinafsi badala ya kujitosa kimasomacho
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka awe ni mfano
hai katika maisha na majitoleo ya Mapadre. Kamwe wasiogope kugharimika na kupata hasara
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika malimwengu!