Maliasili na utajiri wa Sudan ya Kusini vitumike kwa ajili ya mafao ya wengi na maendeleo
endelevu ya wananchi wa Sudan
Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, hivi karibuni
alikuwa ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Parokia ya Mupoi,
iliyoko Sudan ya Kusini. Katika mahubiri yake ameonya kwamba, utajiri wa mafuta uliopo
nchini Sudan, ukitumiwa vyema kwa mafao ya wengi, unaweza kuwa ni kichochea kikubwa
cha maendeleo endelevu, lakini uzoefu unabainisha kuwa mara nyingine utajiri na rasilimali
hizi zimekuwa ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita.
Inasikitisha kuona kwamba,
hata baadhi ya viongozi wa kitaifa waliotopea katika rushwa na ufisadi wanashirikiana
na wawekezaji kutoka nje kwa ajili ya kuwapokonya wananchi utajiri ambao ungetumika
kwa ajili ya mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini katika nchi zao. Utajiri
wa nchi hizi katika takwimu unaonesha kuwa ni mkubwa, lakini watu wake bado wanaendelea
kuogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.
Ni changamoto kwa Serikali
ya Sudan ya Kusini kuhakikisha kwamba, inatumia utajiri wake kwa ajili ya mafao ya
wengi na maendeleo endelevu ya watu wake. Wananchi waendelee kushikamana, kujenga
na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na
changamoto za: utawala bora, mshikamano wa kitaifa, uzalendo na ukakamavu katika ujenzi
wa taifa kwa umoja na upendo. Wananchi wa Sudan ya Kusini, wafahamiane, wapendane
na kuheshimiana kama taifa moja.