2012-12-19 14:29:28

Bikira Maria ni kielelezo cha Imani na Matumaini thabiti kwa ahadi za Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kuwa ni Mama wa Mungu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Katekesi yake katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jumatano tarehe 19 Desemba 2012, ameyaelekeza mawazo yake katika kipindi hiki cha Majilio, kwa kutafakari Imani ya Bikira Maria, Mama wa Kristo.

Malaika Gabrieli aliyetumwa na Mungu kwenda kumpasha habari Bikira Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu, alianza kwa mwaliko kwa Bikira Maria kufurahi kwani Bwana alikuwa pamoja naye. Hii ndiyo furaha ya matumaini ya Kimasiha inayowabubujikia watu wa Mungu na kwa namna ya pekee Binti Sayuni ambaye amejaa neema.

Ni matunda ya neema yanayoujaza Moyo wa Bikira Maria kiasi cha kujaza ile fadhila ya utii kwa Neno la Mungu. Imani ya Bikira Maria kama ilivyokuwa Imani ya Abraham, inafumbata kwa namna ya ajabu imani kwa ahadi za Mungu hata bila kufahamu undani wake. Katika maisha yake, Bikira Maria alifahamu, kama wanavyofahamu waamini wengine kwamba, utashi wa Mungu wakati mwingine unafifia kiasi hata cha kutoweka katika matarajio ya waamini; hali hii anasema Baba Mtakatifu inakumbatia Fumbo la Msalaba.

Ni jambo la muhimu sana kwamba, Bikira Maria anapopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, anafikiri mno moyoni mwake maana ya ujumbe kutoka kwa Malaika Gabrieli. Kwa mfano wa Bikira Maria, waamini wanakumbushwa kuwa imani, licha ya kuwa ni utii kwa utashi wa Mungu, lakini haina budi kuimarisha katika uelewa na kupokea mapenzi ya Mungu kila siku.

Kipindi hiki kitakatifu kinachowaelekeza waamini katika Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, Sala ya Bikira Maria iwasaidie waamini kuwa wanyenyekevu, wanaoamini katika imani inayowafungulia malango ya neema ya Mungu katika mioyo na ulimwengu kwa ujumla. Waamini wajifunze fadhila ya unyenyekevu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu kama alivyofanya Bikira Maria hata akawezeshwa kuwa ni Mama wa Mkombozi; Neno wa Mungu akafanyika mwili.

Bikira Maria ni kielelezo makini cha utii na msikivu wa Neno la Mungu, awawezeshe waamini kujiandaa kikamilifu kumpokea Mkombozi anayekuja kati yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.