Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini amechaguliwa kwa kishindo kuongoza tena cha ANC
kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa kumshinda mpinzani wake Bwana Kgalema Motlanthe
ambaye ni Makamu wa Rais Afrika ya Kusini. Rais Zuma amenyakua kura 2,983 dhidi ya
mpinzani wake aliyejipatia kura 991.
Chama cha ANC kimemchagua pia Bwana Cyril
Ramaphosa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ANC. Huyu ni kati ya "vigogo" wenye utajiri wa
kutisha nchini Afrika ya Kusini; utajiri unaokadiriwa kufikia kiasi cha $675 millioni.
Wajumbe
wapatao 4,000 walikusanyika siku ya Jumanne tarehe 18 Desemba 2012 kuwachagua viongozi
wao kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Uchaguzi huu kadiri ya taarifa za vyombo
vya habari umetanguliwa na vitisho na shutuma za rushwa, lakini hatimaye, ANC imemchagua
Rais Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 70 kuiongoza ANC. Afrika ya Kusini inaendelea
kukabiliana na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na kudumisha mchakato wa ukweli
na upatanisho; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambao unagusa hata viongozi waandamizi
wa Serikali ya Afrika ya Kusini.