Kanisa linaomboleza na kumshukuru Mungu kwa ajili ya Marehemu Askofu mkuu Ambrose
Madtha
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 17 Desemba 2012
aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu
Askofu mkuu Ambrose Madtha, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, aliyefariki
kwa ajali ya gari tarehe 8 Desemba 2012 na kuzikwa Jimboni Mangalore, nchini India
hapo tarehe 14 Desemba 2012.
Katika mahubiri yake, Kardinali Bertone alisema
kuwa Kanisa linaomboleza kifo cha mtumishi wake Askofu mkuu Madtha, mtumishi mwaminifu
na mkomavu, aliyetekeleza utume wake bila ya kujibakiza hata kidogo. Kanisa pia linamshukuru
Mungu kwa zawadi ya Askofu mkuu Madtha ambaye kwa jicho na mwanga wa imani anapumzika
mbele ya Mwenyezi Mungu baada ya kutekeleza wajibu wake, daima akiwa mwaminifu kwa
Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ni changamoto kwa kila mwamini kujiandaa, kukesha
na kusali, daima taa za imani zikiwa zinawaka kwani hakuna anayejua siku wala saa
atakapokuja Mwana wa Mtu, kama ambavyo kifo cha ghafla kilivyomfika Askofu Madtha.
Dhana ya kukesha anasema Kardinali Bertone ni mwaliko wa kuendelea kutekeleza nyajibu
mbali mbali kwa ajili ya kutangaza na kueneza Ufalme wa Mungu na utoaji wa huduma
ya upendo kwa jirani katika uhuru kamili pamoja na kusikiliza Neno la Mungu.
Marehemu
Askofu mkuu Madtha alijitoa kwa unyenyekevu mkuu kusaidia mchakato wa upatanishi miongoni
mwa wananchi wa Pwani ya Pembe waliojikuta wakiogelea katika misigano na kinzani za
kisiasa na kivita. Ni kiongozi aliyependelea kujikita katika majadiliano ya kina kwa
ajili ya mafao ya wengi. Kwa kushirikiana na Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, ameisaidia
Familia ya Mungu kutekeleza wajibu wake barabara katika utoaji wa huduma: kiroho na
kimwili.
Marehemu Askofu mkuu Ambrose Madtha alizaliwa huko Belthangady, India,
kunako tarehe 2 Novemba 1955. Akapadrishwa kunako tarehe 28 Machi 1982. Akaanza huduma
na utume wa Kidiplomasia mjini Vatican mwaka 1990, huko Ghana, El Salvadoro, Georgia,
Albania na China.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 8 Mei 2008
akamteua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, utume ambao ameutekeleza
kwa kipindi cha miaka minne, akiwa bega kwa bega na Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani
ya Pembe katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa nchini
humo.