2012-12-18 08:04:05

Akaunti ya Papa @ Pontifex ina wafuasi zaidi ya millioni mbili!


Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anasema kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya wafuasi millioni mbili ambao wako tayari kwenye akaunti ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwenye mtandao wa Twitter, tangu ulipozinduliwa rasmi hapo tarehe 12 Desemba 2012.

Mitandao ya Kijamii ni Jukwaa linalokusanya umati mkubwa wa watu wanaoishi katika ulimwengu wa mitandao ambao hadi sasa idadi yao inakadiriwa kufikia millioni mia moja na arobaini. Hili ni kundi la vijana wenye umri kati ya miaka kumi na nane hadi thelathini na nne wanaounda asilimia arobaini ya watumiaji wa mitandao ya Kijamii. Haya ni matunda ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yanayowawezesha watu kuwasiliana kwa haraka zaidi. Ni Jamii yenye utamaduni na vipaumbele vyake na kwamba haya ni maskani mapya ya maisha ya binadamu yanayopaswa Kuinjilishwa.

Si haba ndiyo maana hata Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameamua kujiunga na mitandao ya kijamii ili kuwashirikisha watumiaji wa mitandao hii kweli za Kiinjili, hata kwa ujumbe mfupi kabisa. Hapa kinachotakiwa si wingi wa maneno, bali maudhui yaliyomo kwenye maneno haya.

Kanisa linatambua fika uwezo na mapungufu yaliyomo kwenye mitandao ya kijamii. Ni maendeleo ambayo yanagusa sehemu ya watu duniani, lakini katika maeneo kama Bara la Afrika, Amerika ya Kusini na baadhi ya mataifa ya Asia, maendeleo haya yanagusa kundi dogo sana la watu kutokana na sababu mbali mbali. Kutokana na changamoto kama hizi, Kanisa litaendelea kutumia njia mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, watu wanakutana na Habari Njema ya Wokovu pale walipo.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano imeiwezesha Jamii kupata habari nyingi kwa wakati mmoja, kiasi kwamba, wakati mwingine watu wanajikuta wakichanganyikiwa kutokana na mafuriko ya habari zinazowafikia kwa muda mfupi kabisa. Madhara kama haya yanaweza kuwafanya watu kupoteza ladha na utamu wa Injili inayozima kiu na matamanio ya binadamu kutoka katika undani wa maisha yake.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli anabainisha kwamba, hili ni tatizo na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ili kuhakikisha kuwa watu wanaelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, kwa maneno mengine hata Jukwaa la mitandao ya kijamii linapaswa Kuinjilishwa ili kujikita zaidi katika kutafuta mafao ya wengi na maendeleo endelevu ya mwanadamu.









All the contents on this site are copyrighted ©.