2012-12-17 09:10:08

Yaliyojiri katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Imani Katoliki Kaskazini mwa Uganda


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu yuko nchini Uganda kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia moja ya Imani Katoliki Jimbo la Arua na katika Jimbo kuu la Gulu. Aliwasili nchini Uganda tarehe 13 Desemba 2013, akaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa waamini wa Jimbo kuu la Gulu. Akapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kamati ya Ukarabati Kanisa kuu la Arua. Alizindua maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 kwa mashindano ya mpira wa miguu. Alipata nafasi ya kusali masifu ya jioni na Watawa wanaoishi katika Monasteri ya Utatu Mtakatifu.

Tarehe 14 Desemba 2013, Kardinali Filoni na ujumbe wake walifanya hija kwenye Kanisa la Lodonga, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Mapadre pamoja na Watawa wanaoishi na kutekeleza utume wao kwenye Jimbo kuu la Gulu, Uganda. Alipata nafasi ya kutembelea Parokia ya Moyo.

Jumamosi tarehe 15 Desemba 2013 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Waseminari wanaotoka Jimbo kuu la Gulu. Akawakumbusha umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano; dhamana ya Seminari; umuhimu wa kuzingatia muda wa malezi wawapo Seminarini kama kipindi cha kung’amua wito wao, kujifunza na kuboresha maisha yao ya sala na kiroho.

Ni muda wa masomo na fursa makini ya kujenga na kudumisha uhusiano na Yesu Kristo kwa njia ya Ibada kwa Ekaristi Takatifu; kwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kuzingatia mafundisho, wakiwa tayari kuyatolea ushuhuda makini. Anawataka Majandokasisi kuwa shujaa na imara katika imani, wakikumbatia ndani mwao maisha ya useja tayari kuendeleza urithi wa Mama Kanisa kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili Kuinjilisha kwa ari, kasi na moyo mkuu zaidi.

Jioni, Kardinali Filoni alibahatika kuzungumza na baadhi ya Maaskofu Katoliki Uganda, kadiri ya shida zao na baadaye alikutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda na kuwataka kuendeleza ule moyo, kasi na ari ya kimissionari kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kama walivyofanya Mashahidi wa Uganda wanaoheshimiwa na Mama Kanisa.

Wawasaidie waamini kutambua thamani ya utu wao kwa njia ya Injili, ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Maaskofu wajikite zaidi katika kujenga na kuimarisha umoja, haki, amani na upatanisho ili kuondokana na chuki, uhasama na vita ambayo imesababisha mateso na magumu mengi kwa wananchi wa Uganda.

Anawahimiza kukuza na kuimarisha imani, hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Washirikiane kwa karibu zaidi na Mapadri wao katika utekelezaji wa majukumu ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Uganda.

Wawasaidie Watawa kumwilisha karama za mashirika yao katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Wakazie majiundo endelevu kuhusu: Katekesi, Liturujia, Matendo ya huruma kama njia ya kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu, bila kusahau kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa, kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu.

Familia iwe ni Kanisa dogo la nyumbani, wazazi waoneshe mifano bora na utakatifu wa maisha; daima wakiwa waaminifu sanjari na kuthamini utu wa kila mtu. Maaskofu wawe wasimamizi waaminifu wa mali ya Kanisa katika Majimbo yao. Wajichotee utajiri wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Jumapili tarehe 16 Desemba 2012 Kardinali Filoni na ujumbe wake walifanya hija ya kiroho kwenye madhabau ya Indriani pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Tarehe 17 Desemba 2012, Kardinali Fernando Filoni na Ujumbe wake, wameondoka kutoka Gulu kurudi Vatican ili kuendelea na majukumu mengine ya kitume. Haya ndiyo yaliyojiri katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo Jimbo Katoliki Arua, Uganda.








All the contents on this site are copyrighted ©.